Mkutano wa 52 wa Shirika la kimataifa la nishati ya atomiki, IAEA ulifungwa tarehe 4 huko Vienna, Austria. Kwenye mkutano huo wa siku 6, masuala yaliyofuatiliwa zaidi ni jinsi ya kutumia nishati ya nyuklia kwa amani na namna ya kuhakikisha usalama wa nyuklia.
Kwenye ripoti za kazi zilizotolewa na mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Bw. Mohamed El Baradei, zilitaja hatua za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kuhakikisha usalama wa nyuklia, mionzi ya nyuklia na biashara ya teknolojia husika pamoja na usimamizi wa taka za nyuklia, pia hatua hizo zinahusu usimamizi wa ujuzi wa nyuklia, maendeleo ya uzalishaji umeme kwa kutumia nishati ya nyuklia, mageuzi ya teknolojia za nyuklia na uzalishaji maji kwa kutumia kinu cha nyuklia. Kwenye ripoti ya uhakikisho wa usalama wa nyuklia mwaka 2008 inayolenga kukinga ugaidi wa nyuklia, shirika la kimataifa la nishati ya atomiki linatoa wito kwa nchi mbalimbali kuimarisha kazi za kulinda, kufanya upelelezi na kukabiliana na vitendo vyenye nia mbaya kuhusu maliasili za nyuklia na nyingine zenye mionzi, na kuzidisha ushirikiano wa kimataifa katika kukusanya habari zinazohusika.
Kwenye ripoti hizo zilizotolewa na Bw. Baradei, kinachovutia watu ni maelezo kuhusu masuala ya nyuklia ya Korea ya Kaskazini na Iran. Kutokana na Korea ya Kaskazini kutaka kuzindua tena zana zake za nyuklia huko Yongbyon, Bw. Baradei aliitaka nchi hiyo ijiunge tena na makubaliano ya kutosambaza nyuklia haraka iwezekanavyo, hali ambayo itaweka mazingira kwa shirika la kimataifa la nishati ya atomiki kuiingiza Korea ya Kaskazini kwenye mfumo wa kimataifa wa usalama wa nyuklia. Bw. Baradei aliisifu Korea ya Kaskazini kwa msimamo wake wa kufanya ushirikiano. Taarifa hizo zinasema shirika la IAEA linaendelea na ushirikiano na Korea ya Kaskazini, kufanya usimamizi na ukaguzi, na kufuatilia mchakato wa hatua za Korea ya Kaskazini kuondoa uwezo wa zana zake za nyuklia.
Kuhusu suala la nyuklia la Iran, Bw. Baradei alisema bado hajaweza kuondoa uwezekano kuwa Iran inatekeleza kisiri mpango wake wa nyuklia, nae aliitaka Iran iwe na uwazi zaidi katika mambo yanayohusu mpango wake wa nyuklia, na kutangaza hadharani mpango huo haraka iwezekanavyo.
Kitu kingine kinachovutia watu ni kwamba, ripoti zilizotolewa na Bw. Baradei kwa mara nyingine tena zinatoa pendekezo la kuanzisha eneo lisilo na silaha za nyuklia katika Mashariki ya Kati. Ripoti hizo zinatoa wito wa kuchukua hatua za kuongeza hali ya kuaminiana na hatua za ukaguzi, ili kutimiza lengo la kuanzisha eneo lisilo na silaha za nyuklia kwenye sehemu ya Mashariki ya Kati.
Kwenye mkutano huo wa shirika la kimataifa la nishati ya atomiki, mkurugenzi wa shirika la nishati ya atomiki la taifa la China Bw. Chen Qiufa alipotoa hotuba, alieleza mapendekezo ya serikali ya China kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ili kuhimiza matumizi ya nishati ya nyuklia kwa njia ya amani. Vile vile ofisa huyo alifanya mazungumzo na Bw. Baradei kuhusu jinsi ya kuhimiza matumizi ya nishati ya nyuklia kwa amani na usalama. China pia ilitoa mchango wa zana moja ya kukagua usalama wa nyuklia iliyosanifiwa na kutengenezwa na China kwa shirika la kimataifa la nishati ya atomiki, zana hiyo itasaidia shirika hilo katika kutoa mafunzo kuhusu usalama wa nyuklia kwa watu wa nchi mbalimbali.
|