Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-10-08 18:25:49    
Watoto wa kike wa kabila la wahui mkoani Ningxia wapata fursa ya kusoma shuleni

cri

Hivi karibuni mwandishi wetu wa habari alipotembelea katika shule za sekondari za mkoa unaojiendesha wa kabila la wahui wa Ningxia, wanafunzi wa kike hasa wale wanaovaa nguo za kabila la wahui walivutia sana. Imefahamika kuwa, pamoja na utekelezaji wa sera ya kufuta ada za shule za elimu ya lazima ya miaka 9, mkoa wa Ningxia pia umeendelea kutenga fedha zaidi kwa pande mbalimbali za shughuli za elimu vijijini, hasa kuimarisha shughuli za elimu kwa watoto wa kike wa kabila la wahui. Hivi sasa watoto wengi zaidi wa kike wa kabila hilo wamepata fursa ya kusoma shuleni.

Kutokana na kuathiriwa na matatizo ya kiuchumi na mitizamo ya kidini, hali ya elimu ya watoto wa kike wa kabila la wahui ilikuwa iko nyuma sana. Mwandishi wetu wa habari alipotembelea sehemu za vijijini za mkoa huo, aliona kuwa wanawake wengi wenye umri wa zaidi ya miaka 40 walikuwa wamepata elimu ya msingi tu, baadhi yao hata hawakuwahi kusoma shuleni, hali ya uchungu iliyowakumba imewaelimisha wanawake hao ambao wamekuwa na watoto. Mama mzazi wa mwanafunzi Lichunmei wa darasa la sita la shule ya msingi ya wahui ya wilaya ya Xiji ya mji wa Guyuan ana umri wa zaidi ya miaka 50, alisema:

"sikuwahi kusoma shuleni, kwa hiyo maisha yangu yalikuwa na taabu sana. Sasa serikali imeweka sera nzuri na shule zinawafuatilia sana watoto. Nawataka watoto wangu waweze kusoma shuleni, wala wasiwe kama sisi."

Kuanzia majira ya Spring ya mwaka 2006, mkoa wa Ningxia umekuwa mmoja kati ya sehemu zinazofuta ada zote za shule za wanafunzi wanaopewa elimu ya lazima nchini China, hali hiyo ilitoa fursa za elimu kwa watoto wengi hasa watoto wa kike wa familia zenye matatizo ya kiuchumi. Li Chunmei ni mmojawapo.

Mwandishi wetu alipoingia nyumbani kwa Lichunmei, hali ya umaskini kwenye familia yake ilikuwa inaonekana wazi. Imefahamika kuwa, baba yake anapata pato la chini kwa kufanya kazi za vibarua nje, dada zake wawili walikwenda mjini na kufanya kazi katika mikahawa ili waweze kujikimu kimaisha mara baada ya kuhitimu kutoka shule ya msingi. Li Chunmei alisema:

"zamani wakati dada wangu waliposoma shuleni, bado hakukuwa na sera za kufuta ada za masomo, hata hatukuweza kumudu ada za shule. Sasa ada za shule zimefutwa, kila mwaka ninalipa ada za vitabu yuan kadhaa tu. Napaswa kusoma kwa bidii ili niweze kutunza vizuri wazazi wangu katika siku za baadaye."

Mkuu wa shule ya msingi ya wahui ya wilaya ya Xiji ambayo Lichunmei anasoma Bw. Jiang alishika wadhifa huu kuanzia mwaka 1986, alisema:

"mwanzoni mwa miaka ya 80, elimu bado ilikuwa iko nyuma sana. Wakati huo wazazi wengi hawakutilia maanani elimu ya watoto hasa watoto wa kike, na waliona kuwa watoto wa kike hawana haja ya kwenda shuleni. Baadaye kutokana na juhudi za serikali na shule, maendeleo ya uchumi na jamii, mtizamo wa watu kuhusu watoto kwenda shule ulikuwa na mabadiliko makubwa, hasa watoto wa kike pia wana haki sawasawa kama watoto wa kiume ya kupewa elimu ya lazima, kusoma katika sekondari na vyuo vikuu. Sasa idadi ya wanafunzi wa kike na wa kiume katika shule yetu inakwenda kwa uwiano."

Lakini kutokana na sera za kufuta ada za masomo zinatekelezwa kwa elimu ya lazima ya miaka 9 tu, baadhi ya familia zenye matatizo ya kiuchumi bado zinashindwa kumudu ada za shule za sekondari na vyuo vikuu, kuhusu hali hiyo, mkoa wa Ningxia uliongeza uwekezaji kwa elimu, kuihamasisha jamii kutoa misaada wa wanafunzi maskini na kujitahidi kuwapatia watoto wote waliotimia umri wa kwenda shule fursa ya kupata elimu. Mbali na hayo, mkoa wa Ningxia pia umejitahidi kuendeleza mafunzo ya ufundi wa kazi na kuweka njia mpya kwa watoto wa kike kupata elimu na ajira. Ma Yahong mwenye umri wa miaka 20 anatoka sehemu ya maskini iliyoko kusini mwa mkoa wa Ningxia, sasa anasoma usanifu wa mapambo ya majengo kwenye shule moja ya ufundi wa kazi mjini Yinchuan. Ma Yahong anataka kuondokana na umaskini kwa mikono yao na kwa bidii. Alisema:

"natoka wilaya ya Guyuan, nina dada na kaka wengi, wazazi wangu wote ni wakulima, nataka kusoma shule ya sekondari lakini hatuwezi kumudu. Zamani nilikuwa nafanya kazi nyumbani, halafu nikasikia kwamba kusoma katika shule hii ya ufundi kunaungwa mkono wa serikali, natakiwa kulipa yuan 300 tu, baada ya kuhitimu serikali itanipatia ajira. Sitaki kusubiri kuolewa tu nyumbani, nataka kutoka nje kufanya kazi na kupata pesa kusaidia familia yetu. Baada ya kujifunza teknolojia moja nitaweza kufanya kazi mwenyewe bila kutegemea wengine."

Mkoani Ningxia kuna wanawake wengi walioshiriki kwenye mafunzo ya ufundi kama Ma Yahong, kujifunza ufundi fulani na kufanya kazi ni njia inayofaa kwa wasichana wa familia maskini kubana matumizi yao na kujitegemea kiuchumi. Katika shuguli hizo, idara husika za mkoa wa Ningxia pia zimeweka sera maalum zenye nafuu kwa wasichana, mkurugenzi wa idara ya usimamizi wa ufundishaji katika idara ya elimu ya mji wa Yinchuan Bw. Yang Zeting alisema:

"mafunzo yetu kwa wanawake wa kabila la wahui hayana sharti ya umri, hata wanawake wenye umri wa miaka 30 hivi wanaweza kushriki, pia wanaweza kuchagua kwa hiari shule na masomo watakayopenda. Kwa wale wanaotoka familia yenye matatizo ya kiuchumi, tutatoa misaada au kufuta ada zao za masomo ili kuwawezesha wapate elimu bila mizigo."