Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-10-09 16:24:05    
Mabadiliko makubwa ya uchapishaji wa vitabu katika miaka 20 iliyopita nchini China

cri

Kuanzia tarehe mosi mpaka tarehe 4 Septemba tamasha la 15 la kimataifa la vitabu lilifanyika katika mji wa bandari Tianjin. Miaka 22 imepita tangu tamasha hilo lilipoanzishwa mwaka 1986 mpaka sasa, tamasha hilo limekuwa moja ya matamasha manne makubwa ya kimataifa duniani.

Kutokana na kuwa mwanzoni mwa mwezi Septemba kilikuwa ni kipindi cha kufanyika kwa Michezo ya Olimpiki ya Beijing na Michezo ya Olimpiki ya Walemavu, tamasha hilo lilihamia Tianjin, mji ulio karibu na Beijing. Wachapishaji zaidi ya 1,300 kutoka nchi 51 walishiriki kwenye shughuli za tamasha hilo zikiwa ni pamoja na maonesho ya vitabu, biashara ya hakimiliki ya kunakili na mazungumzo kuhusu ushirikiano wa uchapishaji.

Mkurugenzi mkuu wa Kundi la Uchapishaji la China CPG Bw. Li Pengyi aliongoza kundi lake kushiriki kwenye tamasha hilo. CPG ni kundi kubwa la uchapishaji nchini China, chini ya kundi hilo yanakuwepo mashirika 29 ya uchapishaji, maduka 23 ya vitabu na ofisi za shughuli za uchapishaji katika nchi za nje. Kila mwaka kundi hilo linachapisha vitabu vya zaidi ya aina elfu 10 na biashara yake ya hakimiliki ya kunakili zimeenea katika nchi zaidi ya 100. Mwaka 2006 kitabu cha mihadhara ya Yu Dan kuhusu "Maneno Yaliyoteuliwa ya Confuicius' kilichochapishwa nakala milioni tano na Kampuni ya Uchapishaji ya China iliyo chini ya kundi hilo kimevunja rekodi ya historia ya uchapishaji nchini China, kitabu hicho kimetafsiriwa kwa lugha nyingi za kigeni. Bw. Li Pengyi alisema,

"Kampuni ya Macmillan Publishers LTD ya Uingereza imenunua hakimiliki ya kuchapisha kitabu hicho kwa Kiingereza kwa malipo ya kwanza Pauni laki moja, na kitabu hicho cha Kijerumani, Kifaransa, Kiuholanzi, Kiitalia na Kihispania pia kitachapishwa. Mwaka 2009 kitabu hicho cha Kiingereza kitachapishwa katika Ulaya, Amerika ya Kaskazini na Australia. Mwandishi wa kitabu hicho Bi. Yu Dan kwa mwaliko atakwenda Japan, Korea ya Kusini na nchi za Ulaya na Amerika kufanya mihadhara."

Bw. Li Pengyi anaona kuwa katika miaka 30 iliyopita tokea China kuanza kufungua mlango kiuchumi shughuli za uchapishaji nchini China zinaendelea haraka, mashirika mengi yanataka kuanzisha shughuli zao katika nchi za nje na mashirika mengi ya nchi za nje yanataka kuingia nchini China. Tamasha la Kimataifa la Vitabu liliyatolea mashirika hayo firsa ya ushirikiano huo.

Bw. Li Pengyi alisema mwanzoni mwa mwaka 1980 ushirikiano wa ushapishaji na nchi za nje ulikuwa wa mwanzo tu nchini China, wakati huo mkataba wa kwanza wa kuchapisha kitabu cha "Ensiklopedia Fupi ya Kiingereza" kwa ushirikiao na Marekani ulitiwa saini. Huu ni mkataba wa kwanza wa ushirikiano wa uchapishaji kati ya China na nchi za nje kabla ya ushirikiano rasmi wa kimataifa miaka mitatu baadaye. Bw. Li Pengyi alisema,

"Mwaka 1983 mkataba wa kwanza wa ushirikiano wa kuchapisha kitabu cha 'Mwongozo wa Matumizi ya Kiingereza' ulitiwa saini na Chuo Kikuu cha Oxford. Hii ni mara ya kwanza kwa China kushirikiana na mashirika ya uchapishaji ya nchi za nje kwa kuwalipa waandishi wa vitabu."

Tokea hapo katika muda wa miaka 20 hivi biashara ya hakimiliki ya kunakili zimestawi haraka. Mwaka 1992 China imejiunga rasmi na "Makubaliano ya Berne ya Kuhifadhi Hakimiliki Kunakili" na "Makubaliano ya Hakimiliki ya Kunakili Duniani", na China ilianza kuingiza vitabu vingi vya nchi za magharibi. Katika miaka mitano ya mwanzo China ilinunua haki za kunakili 7000, na hadi kufikia mwaka 2003 hakimiliki ya kunakili zilizonunuliwa kutoka nchi za nje zilifikia elfu 12, lakini katika mwaka huo 1992 hakimiliki ya kunakili za vitabu vya China hazikuuzwa 900, hali kama hiyo haiwezi kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya watu wa nchi za nje kutaka kuifahamu China.

Naibu mkurugenzi wa Ofisi ya Habari katika Baraza la Serikali ya China Bw. Li Bing alisema,

"Baada ya mashirika ya uchapishaji ya nchi za nje kutia saini mikataba ya kuchapisha vitabu vya China mashirika hayo yanaweza kupata msaada wa gharama za kutafsiri kutoka ofisi za ubalozi wa China au idara husika nchini China. Hadi sasa China imekuwa na ushirikiano wa uchapishaji na mashirika 108 katika nchi 27, na fedha zinafikia Yuan milioni 30. Katika muda wa miaka miwili tu toka mwaka 2005 hadi 2007, hakimiliki ya kunakili zilizouzwa nchi za nje ziliongezeka na kufikia 2500 kutoka 1400.

Katibu mtendaji wa Chuo Kikuu cha Cambridge Bw. Stephen Bourne alisema ushirikiano na mashirika ya uchapishaji ya China unaleta ufanisi mkubwa. Alisema,

"Katika China tunaweza kupata washirika wanaotufaa, baadhi ya mashirika ya uchapishaji ya China yana uwezo mkubwa wa kusambaza vitabu, na mengine yana sifa za kuchapisha vitabu vya taaluma na vitabu vya elimu kwa ajili ya wanafunzi, na sisi tunayasaidia kwa mahitaji yao.

Katika tamasha hilo pia yalipangwa majadiliano yaliyowashirikisha wataalamu 300 kuhusu "mwelekeo wa ushirikiano wa kimataifa wa uchapishaji". Naibu mkuu wa Ofisi Kuu ya Uchapishaji ya China Bw. Yan Xiaohong alisema, China itaendelea kuimarisha ushirikiano wa uchapishaji na nchi za nje, kuhifadhi na kukamilisha biashara ya hakimiliki ya kunakili. Alisema,

"China itaimarisha ushirikiano huo kwa sera za kuunga mkono mashirika ya uchapishaji nchini kushirikiana na mashirika ya nchi za nje na kutilia nguvu katika mapambano dhidi ya wizi wa hakimiliki ya kunakili, na kuanzisha mfumo wa kupunguza gharama za uchapishaji na kuimarisha huduma za haraka katika biashara ya haki za kunakili na nchi za nje ili na kuleta mazingira bora ya ushirikiano huo wa kimataifa." Bw. Yan Xiaohong aliongeza kwamba hivi sasa serikali ya China inatunga sera hizo.