Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-10-13 20:54:14    
Suala la nyuklia la Peninsula ya Korea lapata maendeleo muhimu

cri
Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje ya Korea ya Kaskazini tarehe 12 Oktoba alikaribisha Marekani kutangaza kuiondoa Korea ya Kaskazini kutoka kwenye orodha yake ya nchi zinazounga mkono ugaidi, ambapo Korea ya Kusini na Japan zimetoa misimamo tofauti juu ya hatua hiyo ya Marekani, na vyombo vya habari vinaona kuwa, hali hiyo inaonesha kuwa suala la nyuklia la Peninsula ya Korea lililokwama limepata maendeleo muhimu.

Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje wa Marekani Bw. Sean McCormack tarehe 11 alitangaza kuwa, kwa kuwa Marekani na Korea ya Kaskazini zimefikia makubaliano kuhusu kukagua na kuthibitisha ripoti ya Korea ya Kaskazini kuhusu mpango wa nyuklia, Marekani iliamua kuiondoa Korea ya Kaskazini kutoka kwenye orodha yake ya nchi zinazounga mkono ugaidi. Bw. McCormack pia alisema Korea ya Kaskazini itaendelea kuondoa uwezo wa kinu cha nyuklia huko Yongbyon, na kuwaruhusu wakaguzi wa Marekani na Shirika la kimataifa la nishati ya atomiki waendelee na kazi yao huko Yongbyon. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya msaidizi wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bw. Christopher Hill na Korea ya Kaskazini, kazi ya ukaguzi na uthibitishaji kuhusu ripoti ya Korea ya Kaskazini ya mpango wa nyuklia inahusu mradi wa Plutonium, na shughuli nyingine za nyuklia za kusafirisha uranium na kuenea kwa silaha za nyuklia. Endapo Marekani na Korea ya Kaskazini zote zitakubali, wataalamu kutoka pande sita wa mazungumzo hayo wataweza kuingia kwenye zana zote za nyuklia zilizotangazwa na zile ambazo bado hazijatangazwa. Pande hizo mbili pia zimekubali kutumia mbinu za kisayansi zikiwa ni pamoja na kuchukua sampuli na madaktari wa mambo ya sheria kufanya upimaji wakati wa hatua hiyo. Bw. McCormack aliongeza kuwa makubaliano hayo yamearifiwa kwa nchi wanachama wengine wa mazungumzo ya pande sita, na utakuwa msingi wa makubaliano kuhusu ukaguzi na uthibitishaji wa ripoti ya Korea ya Kaskazini ya mpango nyuklia yatakayopitishwa kwenye mazungumzo ya pande sita.

Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje ya Korea ya Kaskazini tarehe 12 Oktoba alionesha msimamo wa Korea ya Kaskazini kuhusu hatua hiyo ya Marekani akisema, Marekani imetekeleza ahadi yake kutoa fidia ya kisiasa kwa Korea ya Kaskazini, pia Korea ya Kaskazini na Marekani zimefikia makubaliano kuhusu utaratibu wa ukaguzi na uthibitishaji ulio wa haki na kulingana na madai ya kipindi cha kuondoa uwezo wa majengo ya nyuklia nchini Korea ya Kaskazini. Endapo makubaliano yaliyofikiwa tarehe 3 Oktoba mwaka 2007 kwenye mazungumzo ya pande sita yatakapotekelezwa, Korea ya Kaskazini itachukua msimamo wa kuiunga mkono hatua ya ukaguzi na uthibitishaji yenye lengo la kuondoa uwezo wa kinu cha nyuklia nchini humo.

Siku hiyo Korea ya Kusini na Japan zilionesha misimamo tofauti, ambapo kiongozi wa ujumbe wa Korea ya Kusini Bw. Kim Sook alisema, Korea ya Kusini inakaribisha hatua ya Marekani ya kuiondoa Korea ya Kaskazini kutoka kwenye orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi, na kutarajia kuwa mazungumzo ya pande sita yatafanyika hivi karibuni. Lakini Japan inalalamika kuwa Marekani ilichukua hatua hiyo kabla ya kutatuliwa kwa suala la wajapan kutekwa nyara na Korea ya Kaskazini, na ilieleza kuwa itaendelea kushirikiana na nchi zinazohusika, ili kusaini mapema nyaraka halisi kuhusu kazi ya ukaguzi na uthibitishaji.

Vyombo vya habari vinaona kuwa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani na Korea ya Kaskazini ni maendeleo muhimu yaliyopatikana kwenye suala la nyuklia la Peninsula ya Korea, na kuna uwezekano kuwa mazungumzo ya pande sita yatarejeshwa hivi karibuni, na yatafikia makubaliano kuhusu mipango halisi ya ukaguzi na uthibitishaji.

Lakini wataalamu kadhaa wa Marekani na Korea ya Kusini wanaona kuwa, kuiondoa Korea ya Kaskazini kutoka kwenye orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi ni hatua moja tu kwenye mchakato wa Korea ya Kaskazini kuacha mpango wake wa nyuklia, na mchakato huo bado utakabiliwa na matatizo mbalimbali, na utamalizika baada ya juhudi za miaka mingi. Maofisa wa Marekani pia walieleza kuwa, endapo Korea ya Kaskazini haitaunga mkono hatua ya kukagua na kuthibitisha ripoti yake ya mpango wa nyuklia, Marekani itairejesha kwenye orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi. Ikiwaa ni hivyo, suala la nyuklia la Peninsula ya Korea litakwama tena.