Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-10-15 21:27:49    
Barua 1014

cri

Wasikilizaji wapendwa ni watangazaji wenu Chen na Pili Mwinyi tunawakaribisha katika kipindi hiki cha sanduku la barua. Leo kwanza tunawaletea habari kuhusu kipindi cha chemsha bongo juu ya Vivutio vya Sichuan.

Wasikilizaji wapendwa, tukitaja Mkoa wa Sichuan nchini China labda siyo marafiki wengi wa nje ya China wanaujua, lakini tukitaja Panda, huenda watu wengi wanawapenda wanyama hao wanaoonekana ni wapole sana. Panda wengi kabisa wanaishi mkoa wa Sichuan, kusini magharibi mwa China, Mkoa wa Sichuan ni maskani ya Panda.

Mbali na Panda, katika mkoa wa Sichuan, kuna Bonde la Jiuzhaigou, sehemu hiyo ni kama peponi kwa binadamu; pia kuna Mlima Ermei ambao ni sehemu takatifu ya dini ya Kibudhaa inayojulikana nchini na nje; utamaduni wa sehemu ya Sanxingdui yenye miujiza unawavutia watu wengi; sehemu kubwa yenye mianzi ya Shunan inayopendeza, opera ya Chuan inayoshangaza watu na vyakula mbalimbali vitamu vyote vinawavutia watalii wa nchini na nje.

Kama unataka kueleza zaidi Mkoa wa Sichuan, karibuni katika kipindi maalum cha chemsha bongo kuhusu Vivutio vya Mkoa wa Sichuan, ambapo tutawasomea makala 7 kila wiki kwenye kipindi cha Safari nchini China cha kila jumatatu, na matangazo ya makala yatarudia kwenye kipindi cha Sanduku la barua cha kila jumanne na kila jumamosi.

Kama ilivyokuwa kwenye mashindano ya miaka iliyopita, kila baada ya kusoma makala moja, tutauliza maswali mawili. Baadaye kamati yetu ya uthibitishaji itachagua wasikilizaji washindi wa nafasi ya kwanza, pili na tatu pamoja na nafasi maalum. Washindi watakaopata nafasi za kwanza, pili na tatu watapewa kadi ya kumbukumbu na zawadi; na wasikilizaji washindi watakaopata nafasi maalum wataalikwa kuja China na kutembelea mkoani Sichuan nchini China

Sasa tunawaletea barua tulizotumiwa kutoka kwa wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Geoffrey Wandera Namachi wa sanduku la posta 57333, Nairobi, Kenya ametuletea barua akisema, yeye ni msikilizaji na mfuatiliaji wa matangazo ya Radio China Kimataifa, pamoja na hayo, ameshirikisha wasikilizaji wengi ambao huwa anachukua maoni yao na kuyafikisha kwa waandishi wa habari wa CRI huko Nairobi Kenya.

Leo hii jambo ambalo wasilizaji wengi wamefurahishwa nalo ni kuhusu wakati na masaa ya kupokea matangazo katika saa za Afrika Mashariki. Wasikilizaji wengi ambao amezungumza nao walimdokeza kuwa saa kumi na moja jioni ndio wakati mwafaka wa kusikiliza habari wakiwa wametoka kazini. Wengine walisema kuwa, saa tisa mchana vilikuwa vigumu kwao, kwa vile hawaruhusiwi na wakubwa wao wakiwa kazini. Kwa pamoja wanaipongeza Radio China Kimataifa, kwa kuwajali wasikilizaji wake, kwani hilo limedihirisha kuwa maombi na malalamiko ya wasikilizaji yanazingatiwa zaidi na Radio China Kimataifa.

Mara kwa mara anapoendelea kusikiliza matangazo na kufuatilia vipindi mbalimbali vya CRI, huwa anafurahishwa sana na kipindi cha masimulizi kuhusu vivutio maalumu nchini China. Sehemu hii ya masimulizi ama mazungumzo kuhusu vivutio vya utalii nchini China ni moja wapo ya sehemu ya kutangaza China kuwa mahali pazuri pa kuzuru ama kufanya utalii bora. Ingawa watu wengi duniani hawajawahi kufika China lakini wengi wao wanaifahamu China kutokana na kuwepo kwa matangazo ya Radio China Kiamtaifa CRI pamoja na kukutana na Wachina mbalimbali wakiwemo wawekezaji. Kwa hivyo China inafahamika kwa mambo mengi sana. Ukimuona mchina tayari umeona China kwa jumla na ukiona vitu vinavyotoka China tayari umejuwa ujuzi wa Wachina.

Wasikilizaji wetu wa Kahama CRI Listeners Club P.O.Box 1067 Kahama, Shinyanga, Tanzania wametuletea barua wakishukuru matangazo yetu kuhusu mashindano ya michezo ya 29 ya Olimpiki iliyofanyika mjini Beijing katika Jamhuri ya Watu wa China. Walisema, walisikiliza idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimtaifa kwani inawaelimisha na kuwafundisha mambo mengi mbalimbali yanayotokea kote duniani, vilevile pia na kuwaburudisha. Wanaomba Redio China Kimataifa iwatumie magazeti ya picha yanayohusu mashindano ya michezo ya 29 ya Olimpiki, kalenda za mwaka ujao wa 2009, bahasha pamoja na kadi za salamu. Watafurahi sana ikiwa maobi yao yakikubaliwa na wale wanaohusika wa idhaa ya Kiswahili ya CRI.

Tunamshukuru kwa dhati Geoffrey Wandera Namachi na wasikikilizaji wa Kahama CRI Listeners Club kwa barua zao za kutuelezea juhudi zao za kutusikiliza na kutufuatilia, hii imetutia moyo kuendelea na juhudi za kuchapa kazi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wasikilizaji wetu.

Na sasa tunawaletea mahojiano kati ya mwandishi wetu wa habari na mwanafunzi wa Kenya Ruth anayesoma katika Chuo kikuu cha ualimu cha Tianjin, China.