Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-10-16 16:21:40    
Nyimbo zakuvutia usitake kuondoka mkoani Ningxia China

cri

Mliosikia ni wimbo wa kale unaoenea sana mkoani Ningxia nchini China. Wimbo kama huo unapewa jina la "Hua" maana yake ya kichina ni maua. Wimbo huo ambao unaimbwa kwa miaka mingi miongoni mwa wenyeji unawavutia watu wengi.

Mliosikia ni wimbo mwingine unaoitwa "Machozi yamenitosa macho". Huu ni wimbo unaimbwa sana katika sehemu ya mlimani Liupan, kusini mwa mkoa wa Ningxia. Wimbo huo unaimbwa wakati wenyeji wanapomwaga mgeni.

Katika sehemu ya mlimani Liupan wenyeji wanasimulia kwamba mwanamuziki mashuhuri Bw. Wang Luobin mwaka 1938 alipokuwa safarini kwenda Paris akiwa na dhamira ya kusomea taaluma ya muziki alipita huko na kupumzika katika hosteli moja, alipoondoka mwenye hosteli hiyo Bi. Wu Duomei alimwimbia wimbo huo.

Wimbo huu unasema:

Nakusindikiza kwa macho mpaka upeo wa msisho.

Chakula ubebacho kinapungua kadiri safari upunguavyo.

Nasikia masikitiko, wasiwasi wangu unazidi kuwa mzito.

Machozi yanitosa macho, uchungu waniumiza moyo.

Wimbo mzuri na maneno ya kugusa hisia ulimfahamisha Wang Luobin kuwa muziki mzuri uko huko huko nchini China! Kwa sababu hiyo Bw. Wang Luobin aliacha dhamira yake ya kwenda nchi za nje kujifunza taaluma ya muziki, akabaki mkoani humo akijishughulisha na muziki wa kikabila kwa miaka yote ya maisha yake.

Katika mkoa wa Ningxia, kaskazini-magharibi mwa China, wanaishi watu wa kabila la Wahui, kabila la Wasala na kabila la Wadongxiang. Kati ya makabila hayo lililo kubwa zaidi ni kabila la Wahui ambalo wengi wa kabila hilo ni waumini wa dini ya Kislamu. Watu wa makabila hayo hawana lugha yao wenyewe, wanaongea lugha ya Kichina. Maneno ya nyimbo zao ingawa ni ya Kichina lakini mara nyingi yanachanganywa na maneno fulani ya Kiarabu.

Nyimbo zinazoenea miongoni mwa wakazi mkoani Ningxia hazikutungwa na wanamuziki bali zilitokea miongoni mwa wafanyabiashara walipokuwa katika "njia ya hariri" katika siku za kale, au zilitoka miongoni mwa wavuta mashua kwenye ukingo wa Mto Huanghe.

Nyimbo zote bila kujali zilitokeaje zote zinaeleza mambo ya kimaisha na zinavutia kwa sauti na maneno ya kugusa.

Wimbo huo unasema:

Maua ya mlimani yananukia wakati wote,

Mfereji watiririka bila kukauka mithili mapenzi ya daima,

Kumbuka maneno niliyokunong'oneza,

Tupendane kama chanda na pete.

Wimbo mliosikia unaimbwa sana miongoni mwa wenyeji. Wimbo huo kwanza ulieleza mazingira wanayoishi wenyeji na pia ulieleza hisia zao kutoka kwa mazingira hayo.

Nyimbo zinazosimulia hali ya mazingira kwa kueleza hisia za waimbaji ni nyingi katika mikoa ya Ningxia, mfano mwingine ni wimbo ufuatao.

Wimbo huu unasema:

Maua yachanua kwa furaha,

Msichana ana miaka kumi na saba,

Ameolewa na kaka,

Kila alipomkumbuka machozi yanamlengalenga,

Sababu kaka amesafiri kutafuta maisha,

Anatamani kaka arudi mapema.

Nyimbo za kimapenzi ni sehemu ya utamaduni wa China. Licha ya nyimbo za kimapenzi pia zinakuwapo nyimbo zinazoeleza maisha ya kila siku na ya familia. Sikilizeni wimbo ufuatao:

Wimbo huu unasema:

Ndugu wa familia moja ni kama maji na samaki,

Wanasaidiana kutokana na ndugu wa tumbo moja.

Wakewenza ni kama sahani, zisigongane zinaposafishwa,

Wanafamilia ni misonobari, inavumilia dhoruba kali.

Mwaka 2006 serikali ya China iliweka nyimbo za mkoani Ningxia katika orodha ya urithi wa utamaduni usiooekana wa China, kila mwaka tamasha kubwa la kushindana nyimbo za kikabila hufanyika mkoani Ningxia.

Kabla ya kipindi hiki kumalizika, sikilizeni wimbo uitwao "Karibu pombe mgeni uliyetoka mbali"

Wimbo huu unasema hivi:

Karibu pombe mgeni,

Usiseme pombe si kali,

Huu ni moyo wa urafiki,

Nakutakia salama usalimini.

Idhaa ya kiswahili 2008-10-16