Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-10-24 16:09:18    
Matumizi ya majumba na viwanja vya Michezo ya Olimpiki ya Beijing yahimiza wananchi wa China kujenga mwili

cri
Karibu kila baada ya Michezo ya Olimpiki, miji wenyeji ilikabiliana na matatizo ya uendeshaji wa majumba na viwanja vya michezo, hata baadhi ya miji wenyeji ilibeba mizigo mikubwa ya kiuchumi kutokana na gharama kubwa za ujenzi wa majumba na viwanja hivyo. Michezo ya Olimpiki ya Beijing na Michezo ya Olimpiki ya Walemavu imemalizika, je, Beijing itachukua hatua gani kukabiliana na tatizo hilo? Sasa tunawaletea maelezo halisi.

Bi Li Xiufen mwenye umri wa miaka 62 anaishi katika mtaa wa Shijingshan, mjini Beijing. Kiwanja cha mchezo wa baiskeli cha Laoshan kiko kwenye umbali wa dakika 15 kwa kutembea kwa miguu kutoka kwenye nyumba yake. Wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing, alitazama mashindano ya baiskeli yenye magurudumu madogo ya BMX, na wakati huo alikuwa na matumaini kuwa ataweza kufanya mazoezi ya mwili kwenye kiwanja hicho baada ya Michezo ya Olimpiki. Sasa matumaini yake yametimizwa, alisema:

"Hivi sasa, karibu kila siku mimi pamoja na marafiki kadhaa tunafanya mazoezi ya mwili kwenye kiwanja cha mchezo wa baiskeli cha Laoshan. Hivi sasa mabingwa wa Michezo ya Olimpiki wanafanya mazoezi kwenye kiwanja hicho, na kuna zana mbalimbali mpya za kujenga mwili kama vile mashine ya kukimbia na bwawa la kuogelea, tena bei ya kiwanja hicho ni rahisi, ambayo ni nusu bei kwa sisi wazee. Tunabahatika kupata mazingira mazuri namna hii ya kujenga afya kutokana na Michezo ya Olimpiki."

Wastani wa eneo la uwanja wa kufanya michezo kwa wachina si kubwa, kwa mfano mjini Beijing, takwimu zimeonesha kuwa mwaka 2004 wastani wa eneo hilo la wakazi wa Beijing ni mita za mraba 2.2 tu, lakini nchini Japan kiasi hicho ni mita za mraba 19, na katika nchi za Ulaya na Marekani eneo ni kubwa zaidi. Kutokana na hali hiyo, kufungua majumba na viwanja vyote vya michezo baada ya Michezo ya Olimpiki, ni hatua muhimu ya kuwawezesha watu wengi zaidi kunufaika kutokana na ujenzi wa Michezo ya Olimpiki. Ili kuwashirikisha wananchi wengi zaidi, majumba na viwanja hivyo vya michezo vinafuata kanuni ya kuwahudumia watu, na bei za tiketi ni za chini, hata wanafunzi, wazee na walemavu wanaweza kununua tikekti kwa nusu bei kwenye baadhi ya majumba na viwanja vya michezo. Akizungumzia suala hilo, naibu mkurugenzi wa Idara kuu ya Michezo ya China Bw. Feng Jianzhong alisema:

"Bei za tiketi ya majumba na viwanja hivyo si za juu, kwani lengo letu muhimu ni kuwawezesha wananchi kufanya mazoezi ya mwili kwenye majumba na viwanja hivyo, na bei ya tiketi inawekwa kwa ajili ya kuhakikisha uendeshaji wa kawaida wa majumba na viwanja vya michezo, zikiwa ni pamoja na gharama za nishati, wafanyakazi na vifaa."

Ili kutimiza lengo hilo, na kuhimiza wananchi wote wajenga mwili, Idara ya mazoezi kwenye Idara kuu ya Michezo ya China imefungua majumba na viwanja kwa wananchi baada ya wanamichezo kufanya mazoezi. Mkurugenzi wa idara hiyo Bw. Yan Shiduo alisema:

"Idara yetu imefungua majumba 8 na viwanja 2 vya michezo 17. Michezo hiyo ni pamoja na mipira ya vinyoya, meza, kikapu na wavu na michezo ya tenisi na golf. Isipokuwa Jumapili, viwanja na majumba ya mazoezi ya Timu za taifa la China zinafunguliwa baada ya saa kumi na mbili jioni, na majumba na viwanja vingine vinafunguliwa kwa wananchi kwa siku nzima. Ujenzi na vifaa kwenye majengo hayo vinafikia kiwango cha juu duniani, lakini bei ya tiketi yao ni cha kiwango cha kawaida."

Kuanzia Michezo ya Olimpiki ya Los Angeles ya mwaka 1984 hadi Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008, Idara ya mazoezi imewaandaa mabingwa 120 wa Michezo ya Olimpiki, na idara hiyo pia inachukuliwa kama ni "Mlezi wa mabingwa wa Michezo ya Olimpiki ya China." Kabla ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing, ili kuhakikisha utaratibu wa kawaida wa mazoezi ya timu mbalimbali, Idara ya mazoezi ilifungua tu majumba yasiyo ya mazoezi kwa wananchi, na hivi sasa majumba na viwanja vyote vimefunguliwa.

Baada ya hatua hizo zichukuliwe, wananchi wengi wanafanya mazoezi kwenye majumba na viwanja vya Michezo ya Olmipiki, hali ambayo imeonesha kuwa hatua hiyo imesaidia matumizi ya majumba na viwanja baada ya Michezo ya Olimpiki, pia inahimiza wananchi wa China kujenga afya. Naibu mkurugenzi wa Idara kuu ya Michezo ya China Bw. Feng Jianzhong alisema:

"Serikali imetenga fedha nyingi katika ujenzi wa majumba na viwanja vya michezo, itakuwa na hasara kubwa bila ya matumizi ya kutosha. Ufunguaji wa majumba na viwanja vya michezo kwa wananchi vinawawezesha wananchi kupata fursa ya kuona na kufanya mazoezi kwenye sehemu ambapo mabingwa wa Michezo ya Olimpiki wanafanya mazoezi. Naona kuwa hili ni jambo lenye umuhimu mkubwa kwa jamii na michezo."

Idhaa ya kiswahili 2008-10-24