Wakuu wa nchi 26 wa jumuiya 3 kubwa za Afrika zikiwemo Jumuiya ya Afrika mashariki(EAC), Soko la umoja la Afrika mashariki na kusini(COMESA) pamoja na Jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika(SADC) wamekutana Kampala, mji mkuu wa Uganda wakihudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za jumuiya hizo tatu na kujadili namna ya kuharakisha utandawazi wa uchumi wa Afrika na kutimiza lengo la kuunda umoja wa uchumi wa Afrika. Mchambuzi anasema, utimizaji wa lengo hilo utaanzisha mazingira bora kwa shughuli za biashara kati ya nchi za Afrika na kuongeza nafasi za maendeleo kwa nchi hizo. Hata hivyo, wataalamu wamesema, njia ya kufikia utandawazi wa uchumi wa Afrika ni yenye matatizo mbalimbali.
Nchi 26 za wanachama wa jumuiya tatu za uchumi barani Afrika zinachukua kiasi cha nusu ya idadi ya nchi za Afrika. Idadi ya watu wa nchi wanachama za jumuiya hizo imezidi milioni 500, ikichukua karibu 60% ya idadi ya watu wa Afrika. Thamani ya uzalishaji mali(GDP) kwa wastani wa kila mtu inakaribia dola za kimarekani 1,200. Bw. John Mugerwa, katibu mtendaji wa ofisi ya sekritariati ya Uganda, ambayo ni nchi mwenyekiti wa mkutano huo, alisema, hilo ni soko kubwa na lenye nafasi nyingi za biashara. Endapo jumuiya hizo tatu zitaungana pamoja, basi soko lake litapanuliwa kwa mara kadhaa, nchi zenye nguvu za uchumi za kikanda za Afrika ya Kusini, Kenya, Misri, Liberia na Botswana zilikuwa nchi wanachama wa jumuia tofauti za uchumi, baada ya kuungana pamoja zitaongeza nguvu ya Umoja wa uchumi wa Afrika.
Bw. John Mugerwa alisisitiza, biashara kati ya nchi za Afrika ni za kunufaishana, kwa mfano, Afrika ya Kusini inayoongoza uchumi wa Afrika, hivi sasa inajitahidi kuendeleza teknolojia ya kiwango cha juu, na Kenya ambayo imeendelea zaidi katika kilimo na iko nyuma katika mambo ya viwanda ikilinganishwa nayo, hivi sasa inahitaji sana kuendeleza teknolojia ya upashanaji habari, ni dhahiri kuwa biashara kati ya nchi hizo mbili ni za kunufaishana. Lakini nchi hizi mbili ziko katika jumuiya tofauti za kikanda, shughuli za biashara za nchi hizi mbili zinakabiliwa na vizuizi vingi vya kiutaratibu. Endapo biashara huria inatimizwa, bila shaka itahimiza maendeleo ya uchumi ya pande mbili na nchi hizi mbili zitastawi zaidi.
Mchambuzi anasema, si jambo rahisi kutimiza mpango wa kuunganisha jumuiya hizo tatu. Kwanza, nchi wanachama wa jumuiya hizo tatu zimejiunga na jumuiya zaidi ya moja, katika jumuiya ya COMESA, kuna nchi 4 wanachama ambazo ni nchi wanachama za jumuiya ya EAC, na nchi wanachama 8 ni nchi wanachama za SADC. Jumuiya ya EAC imetimiza umoja wa ushuru wa forodha mwaka 2005, lakini jumuiya ya COMESA inatarajiwa kujiunga na umoja wa ushuru kabla ya mwisho wa mwaka huu, na jumuiya ya SADC itaweza kutimiza lango hilo ifikapo mwaka 2010. Katika wakati mmoja nchi nyingi ni nchi wanachama za jumuiya 2 au jumuiya 3, hivyo ni shida katika upande wa kusawazisha sera za biashara. Pili, msukosuko wa mambo ya fedha ya hivi sasa pia umeathiri kwa kiasi fulani uchumi wa Afrika, nchi nyingi zilizoendelea zimejifunga vibwebwe kukabili msukosuko wa fedha, na zimepunguza misaada ya kiuchumi kwa nchi za Afrika. Pindi biashara huria itakapotimizwa katika sehemu hiyo, bila shaka itazidisha ushindani wa sekta zilizo sawa za nchi wanachama, na huenda itapelekea nchi za Afrika zenye msingi hafifu wa uchumi kukumbwa na matatizo makubwa. Tatu, baada ya kutimizwa biashara huria, viwango vya ushuru wa nchi mbalimbali bila shaka vitashuka, hali ambayo itapunguza pato la serikali linalotoka katika utozaji wa ushuru wa furodha, hii ni moja ya vyanzo vya kuwa na misimamo tofauti kwa viongozi wa nchi mbalimbali kuhusu uunganishaji wa jumuiya hizo tatu. Kutokana na mambo yaliyoelezwa hapo juu, tunaona kuwa njia ya kufikia utandawazi wa uchumi wa Afrika bado ni ndefu, na nchi hizo zinatakiwa kuweka kando tofauti za misimamo yao, na kujitahidi kwa pamoja kutimiza lengo la kustawisha uchumi wa Afrika.
|