Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-10-22 20:27:25    
Ushirikiano kati ya Asia na Ulaya utatoa mchango kwa maendeleo ya dunia

cri

Mkutano wa 7 wa Baraza la wakuu wa Asia na Ulaya utafanyika Beijing kuanzia tarehe 24 hadi 25 mwezi huu. Msaidizi wa waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Liu Jieyi alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema, ushirikiano kati ya Asia na Ulaya katika kukabiliana na msukosuko wa fedha duniani utakuwa suala kubwa litakalojadiliwa zaidi kwenye mkutano huo, na ushirikiano huo utatoa mchango mkubwa kwa ajili ya maendeleo ya dunia nzima.

Kuitishwa kwa mkutano huo katika wakati wa kukabiliwa na hali maalum sana duniani, ambapo msukosuko wa fedha uliosababishwa na msukosuko wa soko la mikopo ya ngazi ya pili nchini Marekani umezidi kuwa mkubwa duniani. Ndiyo maana, China ikiwa nchi mwenyeji wa mkutano huo, imerekebisha kwa wakati mada za mkutano huo, na hali ya uchumi na fedha duniani imekuwa suala kuu litakalojadiliwa kwenye mkutano huo. Bw. Liu Jieyi alisema, kwa kukabiliwa na msukosuko wa fedha wa hivi sasa, nchi mbalimbali za Asia na Ulaya zina maoni ya pamoja na imani imara ya kufanya ushirikiano ili kukabiliana kwa pamoja na matatizo ya hivi sasa. Bw. Liu alisema:

Hivi sasa nchi washiriki wa Baraza la wakuu wa Asia na Ulaya zinajadili kutoa taarifa ya mwenyekiti kuhusu hali ya uchumi na fedha duniani, yaani kueleza nia na dhamiri za nchi za Asia na Ulaya za kufanya juhudi za pamoja katika kukabiliana na msukosuko, kushinda matatizo, na kudumisha ongezeko la uchumi.

Ilifahamika kuwa, mwaka 1997, Bara la Asia lilikumbwa na mgogoro wa fedha, na mwaka wa pili baadaye, mkutano wa pili wa Baraza la wakuu wa Asia na Ulaya uliofanyika huko London, Uingereza ulijadili zaidi sera za kukabiliana na mgogoro huo wa fedha, na kuamua kuanzisha mfuko wa dhamana wa Asia na Ulaya ili kuzisaidia nchi za Asia zirudishe utulivu wa mambo ya fedha na kuondoa athari mbaya ya mgogoro wa fedha kwa jamii. Huu ulikuwa mfano mzuri wa ushirikiano kwenye setka ya fedha. Bw. Liu Jieyi alieleza imani yake kuwa nchi washiriki wa Baraza la wakuu la Asia na Ulaya zitatumia fursa ya mkutano huo kujadili kwa kina zaidi namna ya kuimarisha ushirikiano, kurudisha imani ya wawekezaji na kutafuta njia ya kukabiliana kwa pamoja na msukosuko wa fedha duniani.

Aidha, mkutano huo utajadili masuala magumu mawili kuhusu nishati na mabadiliko ya hali ya hewa, na usalama wa chakula, ambapo washiriki wa mkutano watabadilishana maoni kuhusu ushirikiano katika kuokoa maafa, hali ya Kimataifa na kikanda, kuhimiza biashara na uwekezaji kati ya Asia na Ulaya na maendeleo endelevu.

Bw. Liu Jieyi alisema, mkutano huo unatazamiwa kupitisha "Taarifa ya mwenyekiti" na "Taarifa ya Beijing kuhusu maendeleo endelevu". "Taarifa ya mwenyekiti" itajumuisha misimamo ya viongozi wa nchi mbalimbali kuhusu masuala watakayojadili, maoni yao na juhudi zinazotakiwa kufanya nchi za Asia na Ulaya; "Taarifa ya Beijing kuhusu maendeleo endelevu" itahusu malengo ya maendeleo ya milenia ya Umoja wa Matafia, nishati na mabadiliko ya hali ya hewa, na masikilizano ya jamii, yote hayo yanalenga kukusanya maoni ya pamoja ya nchi za Asia na Ulaya.

Bw. Liu Jieyi alisema, ushirikiano kati ya mabara makubwa ya Asia na Ulaya utatoa mchango mkubwa kwa ajili ya maendeleo ya dunia nzima. Akisema:

Kama mabara hayo makubwa yataweza kufanya ushirikiano na kufanya vizuri mambo ya Asia na Ulaya, ndipo hali ya utulivu itakapopatikana katika nusu ya dunia, na hakika ushirikiano huo utatoa mchango mkubwa sana kwa ajili ya utulivu wa fedha duniani, ongezeko la uchumi na maendeleo ya dunia nzima. Nadhani hii ni sababu ya kimsingi kwa nchi za Asia na Ulaya kukubali kwa kauli moja kuhusu kuimarisha ushirikiano na kujenga kwa pamoja siku nzuri zaidi za mbele kwa ajili ya nchi za Asia na Ulaya.

Habari zinasema kuwa, hivi sasa marais wa nchi au wakuu wa serikali wapatao 38 wamethibitishwa kuwa watahudhuria mkutano wa 7 wa Baraza la wakuu wa Asia na Ulaya.