Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-10-28 19:55:34    
Mazungumzo ya uundaji wa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Zimbabwe yashindwa tena

cri

Mazungumzo ya Harare yaliyoitishwa na umoja wa maendeleo wa kusini mwa Afrika, (SADC) kuhusu suala la Zimbabwe yalishindwa alfajiri ya tarehe 28 kwa saa ya huko. Chama tawala na chama cha upinzani nchini Zimbabwe vilikuwa na mazungumzo marefu ya saa 13, lakini havikuafikiana kuhusu nani atachukua wadhifa wa waziri wa mambo ya ndani ya serikali ya umoja ya nchi hiyo. Kiongozi wa SADC alisema, utaitishwa mkutano wa viongozi wa nchi 15 utakaoshirikisha nchi zote wanachama wa SADC ili kutafuta njia ya kukwamua mazungumzo ya kisiasa ya Zimbabwe. Lakini wakati na mahali pa kufanyika kwa mazungumzo hayo bado havijaamuliwa.

Viongozi muhimu wa sehemu hiyo, ambao ni pamoja na mwenyekiti wa sasa wa SADC ambaye pia ni kaimu rais wa Afrika ya Kusini Kgalema Motlanthe, katibu mkuu mtendaji wa SADC Bw. Tomaz Salomao, rais Armando Emilio Guebuza wa Musumbiji, waziri mkuu wa Swazilan Bw. Barnabas Dlamini, waziri wa mambo ya nje wa Afrika ya Kusini, Bi. Nkosazana Dlamini-Zuma, mratibu aliyeteuliwa na SADC kuhusu mambo ya Zimbabwe, ambaye ni rais wa zamani wa Afrika ya Kusini Bw. Thabo Mbeki walihudhuria mazungumzo hayo.

Kiongozi wa chama cha ZANU-PF, rais Robert Mugabe, kiongozi wa chama cha MDC, ambacho ni chama muhimu cha upinzani ambaye pia ni waziri mkuu mteule Bw. Morgan Tavangirai pamoja na Bw. Mutanbala, kiongozi kutoka chama kingine cha upinzani walishiriki mazungumzo, na walieleza matarajio yao ya kukwamua mazungumzo kwa mashauriano na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa mapema iwezekanavyo, ambapo watu wanayafuatilia mazungumzo kwa shauku kubwa.

Mwakilishi muhimu anayeshiriki mazungumzo wa chama cha ZANU-PF, ambaye alikuwa waziri wa sheria Bw. Chinamasa kabla ya kufanyika kwa mkutano huo, alisema, huenda chama cha ZANU-PF na chama cha MDC vitafikia kwenye mwafaka kuhusu ugawaji wa viti vya mawaziri muhimu. Msemaji wa chama cha MDC, alisema, mazungumzo yamekipa nafasi chama cha MDC, na watatumia nafasi hiyo kueleza tarajio lao la kupata madaraka kwa usawa, pia alieleza wazi malalamiko yao kuhusu baadhi ya hatua zilizochukuliwa na chama cha ZANU-PF. Bw. Thabo Mbeki anaamini kuwa chini ya usuluhisho wa viongozi wa sehemu hiyo, pande mbalimbali husika za Zimbabwe zitaafikiana kwa haraka kuhusu ugawaji wa viti vya mawaziri wa serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo.

Mazungumzo hayo yalipangwa kufanyika tarehe 20 huko Mbabane, mji mkuu wa Swaziland, lakini kiongozi wa chama cha MDC, Bw. Morgan Tsvangirai alikataa kushiriki kwa kisingizio cha kutokuwa na hati rasmi ya kusafiria. Anasema, akiwa waziri mkuu mteule wa Zimbabwe, ni "uonevu" kwake kuwa na hati ya dharura ya kusafiria inayoweza kutumiwa mara moja tu. Alisema pia kuwa chama cha ZANU-PF katika mazungumzo kilikwenda kinyume na kanuni iliyokubaliwa na pande mbili ya kugawanya madaraka, hivyo atasusia mazungumzo yote ya aina hiyo yatakayoitishwa na umoja wa SADC. Maneno hayo ya Bw. Morgan Tsvangirai yanasikitisha watu wengi wa Zimbabwe wanaotarajia kuundwa mapema serikali ya umoja wa kitaifa, watu wa sekta mbalimbali zikiwemo jumuiya ya mawakili, na vyama vya wafanyakazi, wanalaumu maneno na vitendo vya Morgan Tsvangirai vya kususia mkutano, hata imefika hadi kutoa wito wa kutaka chama cha ZANU-PF kiunde serikali peke yake, licha ya hayo, ndani ya chama cha MDC kuna watu wanaotaka kurejesha mazungumzo mapema iwezekanavyo. Mazungumzo ya Swaziland hayakuweza kufanya vizuri majadiliano kutokana na kutoshiriki kwa Bw.Morgan Tsvangirai, viongozi wa umoja wa SADC wamefanya uamuzi kwenye mazungumzo kuendelea na mazungumzo mjini Harare tarehe 27 mwezi huu.