Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-10-29 21:40:23    
Mkutano wa mawaziri wakuu wa China na Russia wafanyika

cri

Waziri mkuu wa China, Bw. Wen Jiabao na waziri mkuu wa Russia, Bw. Vladimir Putin tarehe 28 mwezi Oktoba huko Moscow walihudhuria mkutano wa 13 wa mawaziri wakuu wa China na Russia unaofanyika kila baada ya muda fulani. Pande mbili zilibadilishana maoni kuhusu kuhimiza ushirikiano kati ya China na Russia kwenye maeneo mbalimbali pamoja na masuala muhimu ya kimataifa na kikanda zinayoyafuatilia, na zilikuwa na maoni ya namna moja.

"Mkutano wa 13 wa mawaziri wakuu wa China na Russia unafanyika juu ya msingi wa uhusiano wa kiwenzi na kimkakati wa China na Russia, na katika hali ambayo kuna msukosuko wa uchumi na fedha humu duniani, hivyo mkutano huu ni muhimu na unafuatiliwa sana na watu."

Baada ya kujadiliana kwa saa 2, waziri mkuu Wen na waziri mkuu Putin walikutana na waandishi wa habari. Waziri mkuu Wen alisisitiza, katika mazingira ya hivi sasa yenye utatanishi na mabadiliko mengi na kuweko kwa msukosuko wa mambo ya fedha duniani, kuimarisha uhusiano wa kiwenzi na kimkakati wa China na Russia ni muhimu sana kwa kulinda maslahi za nchi mbili na kuhifadhi amani na utulivu wa dunia.

Bw. Wen Jiabao alisema, alijadiliana kwa kina na waziri mkuu Putin kuhusu ushirikiano wa nchi mbili kwenye maeneo mbalimbali pamoja na masuala muhimu ya kimataifa na kikanda, na kufikia kwenye mwafaka. Hii ni muhimu sana kwa uhusiano wa urafiki na ushirikiano wa hivi sasa kati ya nchi hizi mbili, bali pia ni muhimu sana kwa maendeleo ya muda mrefu ya uhusiano wa nchi mbili.

"Juu ya msingi wa kuheshimiana, kuwa na usawa na wa kunufaishana, uhusiano wa China na Russia unahusu mambo ya uchumi, biashara na fedha, pamoja na mambo ya utamaduni. Hususan, mkutano huu umetilia mkazo katika shughuli za uchumi na biashara, kukabiliana na msukosuko wa fedha na kuimarisha ushirikiano katika mambo ya fedha. Ninaamini, hii itaimarisha utulivu wa uchumi, mambo ya fedha na masoko ya mitaji ya nchi mbili, na itachangia maendeleo ya uchumi wa pande mbili."

Bw. Putin alisifu sana uhusiano wa kiwenzi na kimkakati kati ya China na Russia, alisema, Russia inapenda kushirikiana na China, kutumia vilivyo mifumo mbalimbali ya nchi mbili, kusawazisha misimamo na kuimarisha ushirikiano kuhusu maswala muhimu, kuhimiza maingiliano ya kirafiki na ushirikiano katika maeneo mbalimbali. Alisema:

"Katika dunia ya hivi leo, ni vigumu kwa sisi kupata nchi yenye mambo mengi ya ushirikiano na mifumo mizuri ya uratibu kama ya China, aidha, ushirikiano wetu katika maeneo mbalimbali umekuwa ukiimarishwa. Tunaona, pande mbili zinatakiwa kutumia vizuri fursa ya ushirikiano katika maeneo mbalimbali."

Mbali na hayo, pande mbili za China na Russia zinakubali kuinua ufanisi na kiwango cha ushirikiano wa uchumi na biashara, kuimarisha ushirikiano kwenye maeneo ya maendeleo ya sayansi na tekinolojia yakiwemo ya safari ya chombo kwenye anga ya juu, usafiri wa ndege na aina mpya za vifaa, kuendelea kuhimiza ushirikiano kwenye maeneo ya mafuta ya petroli na gesi ya asili, uzalishaji wa umeme na uzalishaji wa umeme kwa nguvu za nyukilia, na kuhimiza kwa pande zote ushirikiano kwenye sekta ya utamaduni, kuratibu mikakati ya maendeleo ya kikanda na kuendelea kuimarisha uratibu na ushirikiano wa pande mbili katika mambo ya kimataifa na kikanda.

Baada ya mkutano, mawaziri wakuu hao walisaini taarifa kuhusu mkutano huo wa 13, na kushiriki kwa pamoja sherehe ya utiaji sahihi wa nyaraka nyingi za ushirikiano.