Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-10-30 20:25:26    
Tetemeko la ardhi latokea Pakistan

cri

Tetemeko kubwa la ardhi la nguvu ya 6.5 kwenye kipimo cha Richter lilitokea tarehe 29 katika mkoa wa Baluchistan, sehemu ya kusini magharibi nchini Pakistan, na limesababisha vifo vya watu wengi na hasara kubwa ya mali. Hivi sasa, serikali ya Pakistan inajitahidi kadiri iwezavyo kupunguza hasara inayosababishwa na maafa hayo.

Kitovu cha tetemeko hilo kiko kwenye sehemu ya milima karibu na Quetta, mji mkuu wa mkoa wa Baluchistan, nyumba zaidi ya 1,000 za mjini Qutta zilibomoka.

Tetemeko la ardhi limesababisha vifo vingi vya watu na hasara kubwa ya mali. Ofisa wa huko alisema, wakazi elfu 46 walikumbwa na maafa hayo, zaidi ya vijiji 8 vya huko viliathirika zaidi. Mkuu wa idara ya uratibu na uongozi wa kazi za kupunguza hasara ya maafa, Bw. Farooq Ahmed Khan siku hiyo alitangaza, watu 115 wamethibitishwa kuwa walikufa katika maafa, kiasi cha watu 300 walijeruhiwa, hivi sasa kuna watu wengi waliofukiwa chini ya vifusi, hivyo kazi za uokoaji bado zinaendelea, na idadi ya vifo vya watu na majeruhi huenda itaendelea kuongezeka. Televisheni binafsi ya huko ilitangaza kuwa idadi ya vifo vya watu katika maafa hayo imezidi 200.

Hali ya maafa ya tetemeko la ardhi inafuatiliwa sana na viongozi wa Pakistan. Rais Asif Ali Zardari na waziri mkuu wa nchi hiyo, Bw. Yousuf Raza Gilani, ambaye hivi sasa yuko ziarani nchini Uturuki, walitoa salamu za rambirambi kwa watu waliokubwa na maafa, na kutaka serikali kuu na za mikoa zijitahidi kadiri ziwezavyo kuwasaidia watu walioathirika katika maafa, na kutoa misaada ya matibabu kwa majeruhi. Bw. Gilani alisema, serikali itatoa fidia za rupee laki 3 (ambapo dola 1 ya kimarekani ni sawa na rupee 80) kwa jamaa za marehemu, na kutoa msaada wa rupee laki 1 kwa kila mjeruhi.

Mara tu baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi, serikali ya huko na idara za matibabu zilifanya haraka kazi za utoaji misaada, zimejenga mahema kwenye sehemu zilizokumbwa na maafa yakiwa kama hospitali za muda na kuwatibu majeruhi, wakati baadhi ya majeruhi wengine walihamishwa katika hospitali za karibu, jeshi la nchi hiyo limetuma helikopita 12 kushiriki katika kazi za uokoaji. Mkuu wa idara ya uratibu na uongozi wa kazi za kupunguza hasara ya maafa, Bw. Farooq alisema, idara yake imekusanya mahema 2,000 katika mji wa Quetta na mablanketi mengi kutoka sehemu nyingine, sasa vitu hivyo vimepelekwa kwenye sehemu zilizoathirika. Hospitali 1 inayozunguka katika sehemu mbalimbali imepelekwa kwa ndege hadi sehemu moja iliyoathirika vibaya kutoka Rawalpindi, hivi sasa hospitali nyingine moja ya aina hiyo imejiweka tayari, na inaweza kuhamishwa kwenye sehemu nyingine katika wakati wowote.

Ingawa serikali ya Pakistan inajitahidi kupunguza hasara ya maafa, lakini watu walioathirika bado wanakabiliwa na matatizo mawili makubwa. La kwanza, kutokana na kubomoka kwa nyumba zao katika tetemeko la ardhi, sasa hawana mahali pa kujisetiri katika usiku wenye baridi kali, maofisa wa huko wametoa ombi kwa serikali kuwaletea mahema elfu 10 pamoja na zana za kupasha joto. Pili, matetemeko mengine madogo yanatokea mara kwa mara kwenye sehemu hizo, maporomoko ya mawe na udongo yanatishia usalama wa maisha ya watu walionusurika na waokoaji.

Hali ya maafa ya nchini Pakistan inafuatiliwa na kuhurumiwa na jamii ya kimataifa. Baada ya kutokea kwa maafa hayo, rais Hu Jintao na waziri mkuu Wen Jiabao wa China walitoa salamu za dhati kwa serikali ya Pakistan na wananchi wake, na kutoa maombolezo kwa watu waliofariki katika maafa. Baadhi ya nchi ikiwemo Marekani na jumuiya za kimataifa zimeahidi kutoa misaada kwa Pakistan. Hususan serikali ya India, iliahidi kwa haraka kutoa misaada kwa Pakistan. Hivi sasa kamati ya msalaba mwekundu ya duniani imetuma vikundi viwili kwenda kufanya uchunguzi kuhusu hali ya sehemu zilizokubwa na maafa, na mahitaji ya watu waliokubwa na maafa. Chini ya uongozi wa serikali ya Pakistan na misaada ya jamii ya kimataifa, watu wanaamini kuwa watu waliokumbwa na maafa ya tetemeko la ardhi nchini Pakistan, wanaweza kushinda shida mbalimbali na kujenga upya maskani zao.