Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-10-30 19:49:40    
Utenzi wa kwanza katika historia ya fasihi ya China "Tausi Arukia Kusini Mashariki"

cri

"Tausi Arukia Kusini Mashariki" ni utenzi wa kwanza kabisa katika historia ya fasihi ya China, na ni moja kati ya maandishi maarufu ya fasihi ya China. Utenzi huo ulitokea katika kipindi cha Enzi ya Kusini iliyoanzia mwaka 420 hadi 589, asili yake ilikuwa ni utunzi miongoni mwa wenyeji katika Kipindi cha Jian An kilichoanzia mwaka 196 hadi mwaka 220 na baadaye ulirekebishwa katika muda mrefu. Utenzi huo una beti zaidi ya 350 zenye maneno zaidi ya 1,700, mambo yanayoelezwa ni hadithi ya mapenzi yanayosikitisha iliyotokea katika zama za kale nchini China.

Kwa ufupi, hadithi inaeleza kwamba, katika siku za kale kulikuwa na mume na mke ambao wote ni vijana. Msichana aliitwa Liu Lanzhi ambaye alikuwa mpole, mwerevu na ni hodari wa kazi za nyumbani. Ili kuendesha vizuri maisha, bibi huyo kila siku alikuwa anashughulika toka asubuhi mapema mpaka usiku bila kupumzika, hata hivyo alichukizwa na mama mkwe wake na mara kwa mara alikaripiwa na kutukanwa. Kutokana na hali hiyo bibi huyo alitaka kurudi nyumbani kwa mama yake mzazi. Mume wake Jiao Zhongqing ambaye alikuwa ofisa na hakai nyumbani kila wakati, baada ya kusikia habari hiyo mara alirudi nyumbani na kumshawishi mama yake akisema mwanamke mzuri kama mke wake Liu Lanzhi hapatikani tena, kama mkewe akiondoka yeye hataoa tena. Baada ya kusikia hayo kinyume na kushawishika, mama yake alikasirika sana, aling'ang'ania kumlazimisha mwanawe amrudishe mkewe nyumbani kwao. Jiao Zhongqing mwenye utiifu kwa mama yake alikuwa hana budi kumbembeleza mkewe akimwambia arudi nyumbani kwa muda fulani mpaka hasira zitakapomtoka mama yake. Lakini mkewe Liu Lanzhi alielewa moyoni kwamba chuki za mama mkwe hazikupatikana kwa siku moja na haziwezi kumtoka kwa siku chache, akatoa zawadi alizopewa na mama yake mzazi alipoolewa akampa mumewe kama ni kumbukumbu huku akiwa amerowa machozi. Siku ya pili baada ya kujivalia na kujipamba vizuri alimuwaga mama mkwe wake na kuanza safari ya kurudi nyumbani kwa mama yake mzazi kwa mkokoteni, mumewe alitangulia mbele kwa farasi na yeye alimfuata nyuma, mume na mke hao wawili walijawa na simanzi. Kabla ya kuondoka nyumbani wapenzi hao waliahidiana kwamba hata wakiwa na hali gani basi hawataachana na kuwa na ndoa nyingine.

Baada ya kurudi nyumbani kwa mama yake mzazi, Bibi Liu Lanzhi alimkumbuka sana mumewe usiku na mchana, ingawa mara nyingi walikuja washenga kumposa kutokana na uzuri wake, lakini kila mara alikataa kwa maneno mazuri, mwishowe kukataa kwake kulimhamakisha kaka yake. Liu Lanzhi alifikiri kwamba kuishi tena na mume wake mpenzi ni muhali kabisa, hivyo alikubali ndoa. Kusikia habari hiyo Jiao Zhongqing kwa haraka alikwenda kwa mkewe na kwa huzuni na hasira alimwuliza kwa nini alivunja ahadi na kutamani maisha ya anasa. Liu Lanzhi aliyekosewa kuelewa alishindwa kusema kitu ila kumpa mumewe buriani ya mwisho. Baada ya kurudi nyumbani Jiao Zhongqing alimshawishi tena mama yake lakini mama huyo alishikilia uzi ule ule bila kulegeza. Kutokana na ukaidi wa mama yake Jiao Zhongqing aliamua kujiua. Katika siku ya harusi Liu Lanzhi alijitosa, na Jiao Zhongqing alijinyonga. Wapenzi hao wawili wamekwenda ahera na kuacha hadithi yao ya kusikitisha duniani. Jinsi vijana hao walivyopendana kwa uaminifu iliwazindua wazazi wao, wakawazika pamoja na walipanda misonobari kwenye kaburi lao, inasemekana kwamba baadaye walitokea ndege wawili wakiorukaruka kwenye miti bila kutaka kuondoka.

Hadithi ya "Tausi Arukia Kusini Mashariki" licha ya kuwasikitisha wasomaji pia inawaasa wathamini mapenzi yao na wasijitafutie masikitiko.