Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-10-30 19:53:59    
Mwongozaji wa filamu za hifadhi ya mazingira Bw. Feng Xiaoning

cri

Mwezi Oktoba filamu ya "Kimbunga Kikali" imekuwa ikioneshwa kila mahali nchini China. Filamu hiyo iliyogharimu Yuan milioni 50 katika matengenezo yake inagusa hisia za watazamaji kwa nguvu. Inafahamika kwamba filamu hiyo imechaguliwa kuwa mojawapo ya filamu zinazooneshwa katika Tamasha la 21 la Kimataifa la Filamu mjini Tokyo. Hii ni filamu yake nyingine aliyopiga Bw. Feng Xiaogang hivi karibuni kwa nia ya kuwaasa watu wawe na fikra za kuhifadhi mazingira.

Filamu ya "Kimbunga Kikali" ilihaririwa kwa mujibu wa kimbunga kiitwacho "Saomai" kilivyokumba mji wa Wenzhou, mji wa pwani nchini China mwaka 2006, na ikieleza jinsi serikali ya mji wa Haitong ilivyowashirikisha wakazi kuukimbia haraka mji huo wakati kimbunga cha "Nyangumi Buluu" kilipokaribia kufika mji huo mwaka 2006. Filamu hiyo inagusa kwa nguvu hisia za watazamaji kutokana na mawimbi makali, nguvu kubwa za pepo za chamchela na utulivu wa ajabu kwenye sehemu ya katikati ya kimbunga. Watazamaji wanashuhudia jinsi mji mmoja ulio mzuri ulivyotoweka kwa dakika chache na jinsi malimioni ya wakazi walivyohamishwa kwa dharura kutoka sehemu zilizokumbwa na maafa.

Bw. Feng Xiaoning alisema, filamu hiyo inaonesha maana yake nzito kwa kuwakumbusha watu wasipuuze maafa ya kimaumbile na wawe tayari kupambana na maafa hayo. Alisema,

"Filamu ya 'Kimbunga Kikali' imeonesha maafa makubwa ya kimaumbile, na maafa hayo yamewaletea Wachina kovu kubwa mioyoni mwao. Maafa kama ya theluji na barafu, matetemeko ya ardhi, mafuriko na mengi mengineyo ya kimaumbile ni matukio makubwa katika maisha ya binadamu, ni maafa yanayoikumba dunia nzima. Wakati tulipopiga filamu hiyo ndipo kimbunga kiitwacho "Katrina" kilipoikumba Marekani. Filamu yangu inawaambia Wachina na hata watu wa dunia nzima kuwa watafikiwa kwa lazima zama za maafa hayo ya maangamizi. Katika filamu yangu hii nimethibitisha kwamba maafa ya maumbile yanaletwa na sisi binadamu wenyewe kutokana na kuharibu mazingira na kusababisha kuongezeka kwa joto duniani."

Bw. Feng Xiaoning alizaliwa miaka 50 iliyopita na alihitimu katika Chuo Kikuu cha Filamu cha Beijing, ambapo alichukua kozi ya upigaji filamu lakini baadaye amekuwa mwongozaji. Filamu alizoongoza kupigwa, nyingi ni za kivita, lakini pia anazingatia tatizo la hifadhi ya mazingira. Anaona kwamba uharibifu wa mazingira ni hatari inayofichika, na uharibifu wake si mdogo ikilinganishwa na vita. Vita haiwezi kuiangamiza China lakini uharibifu wa mazingira unaweza kuiangamiza China na hata dunia nzima.

Mwaka 2000 Bw. Feng Xiaoning alipiga filamu ya "Shujaa Gada Meilin". Hii ni filamu inayoeleza shujaa wa Kabila la Wamongolia la China alivyopambana na uharibifu wa nyika za malisho, na jinsi watu walivyonyakuana eneo lililobaki la malisho.

Mwaka 2003 Bw. Feng Xiaoning alipewa jina la heshima la "balozi wa hifadhi ya mazingira" wa China na Shirikisho la China la Hifadhi ya Mazingira, na mwaka 2007 alipata heshima nyingine ya "Mhifadhi Mazingira wa China Mwaka 2007". Katika muda wa miaka 20 ya upigaji wake wa filamu alisafiri karibu kila mahali nchini China lakini hakufanya uharibifu wowote wa mazingira, na watu wa kundi lake hawakuwahi kutupa ovyo takataka. Mwaka 2006 alipopiga filamu na kundi lake katika nyika za Kekexili zenye mwinuko wa mita 5000 kutoka usawa wa bahari watu waliovuta sigara walikuwa hutia vipande vya mwisho vya sigara ndani ya paketi. Kila baada ya siku ya shughuli za kupiga filamu kumalizika, watu wa kundi lake walikuwa hujituma kusafisha takataka walizoacha, na magari yao yanakimbia tu kwenye barabara bila kukanyaga majani. Kabla ya hapo, Bw. Feng Xiaoning alikuwa huwaasa wenzake wasiharibu mazingira, lakini baadaye aligundua kwamba onyo lake halina haja.

Bw. Feng Xiaoning alisema, filamu atakazopiga zitakuwa za kibiashara zaidi lakini atatia maanani filamu za kuhifadhi mazingira. Alisema,

"Filamu ya 'Kutoweka kwa hewa ya anga ya juu' ni filamu yangu niliyopiga miaka 20 iliyopita, hii ni filamu nzuri kwa hadithi yake ya ajabu na maudhui yake, hata ikioneshwa sasa bado inavutia sana ingawa miaka 20 imepita. Maudhui ya filamu hiyo ni sawa na filamu yangu ya sasa 'Kimbunba Kikali', kwamba zote zinawaasa binadamu waishi kwa amani na dunia ya maumbile, wala sio kupambana na dunia ya maumbile. Hapo zamani Wachina hawakufahamu suala hilo, walipambana na dunia ya maumbile badala ya kuishi nayo katika hali ya mapatano, wakapata mafunzo makubwa. Sasa tumeelewa kwamba binadamu lazima wawe na ubinadamu kwa dunia ya maumbile."