Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-10-31 16:20:33    
Mabadiliko ya shughuli za fedha katika miaka 30 iliyopita tangu China ianze kutekeleza sera ya mageuzi na ufunguaji mlango

cri

Katika miaka 30 iliyopita tangu China ianze kutekeleza sera ya mageuzi na ufungaji mlango, mabadiliko makubwa yametokea katika shughuli mbalimbali za kiuchumi nchini China, ikiwemo shughuli za fedha. Masoko ya hisa ya China yamepata maendeleo hatua kwa hatua, mabenki yanatoa huduma bora za aina nyingi; watu wa kawaida wananufaika na bima, wakiwemo wakulima wanaoishi kwenye sehemu za mbali na vijijini.

Bibi Chen Fan ni mkazi wa Beijing mwenye umri wa miaka 51. Alianza kununua hisa kabla ya miaka 9 iliyopita. Kila siku anafuatilia soko la hisa, alisema,

"Kila siku baada ya kufanya mazoezi ya kujenga mwili katika bustani, ninarudi nyumbani, kuwasha komputa yangu, na kusoma habari kuhusu hali ya soko la hisa kwenye mtandao wa Internet. Kama bei za hisa zinapanda juu, huwa napiga simu kuuza hisa hizo. Ninapanga kuomba huduma ya kufanya biashara ya hisa kupitia mtandao wa Internet, kwa sababu ni rahisi zaidi kuuza na kununua hisa kwenye mtandao wa Internet."

Bibi Chen ni mmoja kati ya Wachina karibu milioni 100 wanaofanya biashara ya hisa. Hivi sasa hali ya hisa ni jambo linalojadiliwa zaidi na watu wa China. Lakini katika miaka 30 iliyopita, watu waliojua hisa ni wachache, na watu waliojua soko la hisa ni wachache zaidi. Wakati huo, kutokana na kutekelezwa kwa sera ya mageuzi na ufunguaji mlango, masoko ya hisa yalianza kutokea nchini China.

Mwaka 1984, serikali ya China iliruhusu wafanyakazi kununua hisa za makampuni yao na kupata faida katika mwishoni mwa mwaka. Baadhi ya makampuni ya miji ya Beijing na Shanghai, na mikoa ya Guangdong, Sichuan na Liaoning yalianza kufanya majaribio ya utaratibu wa kuchangia hisa. Mwezi Novemba mwaka huo, hisa ya "vyombo vya umeme vya muziki vya Feiyue" ilianza kuuzwa, ambayo imekuwa hisa ya kwanza iliyouzwa baada ya China kutekeleza sera ya mageuzi na ufunguaji mlango.

Baadaye masoko ya hisa ya China yalipata maendeleo ya haraka. Katika miaka ya 90 ya karne iliyopita, ilikuwa ni lazima watu wanunue na kuuza hisa katika jumba la biashara ya hisa ambapo ilisababisha msongamano mkubwa wa watu, na waliweza kununua hisa za aina zaidi ya 10 tu. Lakini hivi sasa makampuni yanayouza hisa zao katika masoko ya Shanghai na Shenzhen ni zaidi ya 1800, ofisi za biashara ya hisa zimetapkaa katika miji mbalimbali. Watu wengi wanafanya biashara ya hisa kupitia simu na mtandao wa Internet.

Kutokana na kupanda kwa thamani ya hisa za makampuni ya China, thamani ya hisa zinazouzwa katika masoko ya Shanghai na Shenzhen ziliwahi kufikia yuan trilioni 30. Prof. He Qiang wa Chuo Kikuu cha Fedha na Uchumi cha China anaona kuwa, sifa za makampuni zinazouza hisa zao masokoni zinainuliwa siku hadi siku, akisema,

"Kwa kweli muda mfupi baada ya masoko ya hisa kuanzishwa nchini China, sifa za makampuni mengi yaliyouza hisa zao masokoni hazikuwa nzuri. Lakini tumerekebisha utaratibu wa uuzaji wa hisa masokoni, na kuinua uidhinishaji wa makampuni yanayouza hisa masokoni, hivyo sifa za makampuni zimeinuliwa. Makampuni ni msingi wa masoko ya hisa, sifa na maendeleo mazuri ya makampuni yataweka msingi imara kwa maendeleo ya masoko ya hisa."

Mageuzi ya idara mbalimbali za shughuli ya fedha zinafanyika nchini China. Kwa mfano, katika miaka 30 iliyopita, maendeleo ya uchumi na mabadiliko ya mahitaji ya fedha yameyahimiza mabenki yatoe huduma za aina mbalimbali ambazo ni rahisi kupata. Hadi mwishoni mwa mwaka jana, mabenki 78 yalitoa huduma ya kushughulikia mali binafsi, ambayo yanachukua zaidi ya asilimia 70 ya mabenki ya China. Thamani ya uuzaji wa huduma hiyo ilifikia yuan bilioni 819, na katika robo ya kwanza ya mwaka huu, thamani hiyo imekuwa kubwa zaidi kuliko thamani ya uuzaji ya mwaka jana mzima uliopita.

Mwandishi wetu wa habari aliona huduma ya kushughulikia mali za muda mfupi iitwayo "Lingtongkuaixian" kwenye tawi moja la Benki ya Viwanda na Biashara ya China. Kiongozi wa tawi hilo Bi. Zhao Na alisema,

"Thamani ya uuzaji wa huduma ya kushughulikia mali za muda mfupi ya Lingtongkuaixian inachukua nusu ya thamani ya uuzaji wa huduma za kushughulikia mali za benki yetu, kwa sababu huduma hiyo inafaa watu wanaoshughulikia mali za muda mfupi."

Mabenki ya China yakichukua fursa ya China kushiriki kwenye Shirika la Biashara Duniani, yanafungua mlango hatua kwa hatua kwa nje. Mwaka 2007, China ilikubali rasmi maombi ya mabenki ya nje kuhusu kushughulikia kadi za fedha za kigeni na za Renminbi. Mwezi Aprili mwaka huo, mabenki ya Standard Chartered, HSBC, BEA na Citibank zilipata uidhinishaji wa kuanzisha shughuli zote za fedha nchini China. Viongozi wa mabenk hayo walisema wana matumaini kuwa watatoa huduma bora kwa Wachina. Meneja mkuu mtendaji wa benki ya Standard Chartered Bw. Peter Sands alisema,

"Sitaweka vikwazo vyovyote, tutatoa huduma kwa mujibu wa mahitaji ya Wachina. Tutatoa huduma sawa na tunazotoa katika nchi nyingine."

Shughuli ya bima ikiwa ni shughuli muhimu ya kiuchumi, ilikuwa jambo lililojulikana kwa watu wachache katika miaka 30 iliyopita. Na hivi sasa imekuwa jambo muhimu kwenye uchumi wa jamii ya China na maisha ya watu wa kawaida.

Wakati China ilipoanza kutekeleza sera ya mageuzi na ufunguaji mlango, nchini China kulikuwa na kampuni moja tu ya bima, ambayo mapato ya kampuni hiyo yalikuwa yuan milioni 460. Hadi kufikia mwaka 2007, makampuni ya bima ya China yalifikia 110, na mapato ya makampuni hayo ilikuwa yuan bilioni 700. China imekuwa ni nchi ambayo shughuli zake za bima zinastawi.

Shughuli za fedha za China zimepata maendeleo makubwa ambayo yanafuatiliwa na dunia nzima katika miaka 30 iliyopita. Lakini wataalamu walisema mageuzi ya shughuli za fedha za China ambazo zina dosari mbalimbali bado ni kazi ngumu na ya muda mrefu, ili shughuli hizo ziweze kukabiliana na mwelekeo na changamoto mpya duniani.