Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-10-31 18:14:04    
Baraza kuu la Umoja wa Mataifa laitisha mkutano maalumu kunasua msukosuko wa fedha

cri

Baraza kuu la 63 la Umoja wa Mataifa liliitisha mkutano maalumu tarehe 30 mwezi Oktoba katika makao makuu yake mjini New York, washiriki wa nchi mbalimbali pamoja na wataalamu wa uchumi wanajadili mbinu za kunasua msukosuko wa fedha uliopo hivi sasa duniani, na namna ya kutathimini mfumo wa mambo ya fedha wa dunia. Washiriki wanasema, dunia inapaswa kufanya mageuzi kuhusu mfumo wa mambo ya fedha uliopo hivi sasa.

Mwenyekiti wa sasa wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa, Bw. Miguel d' Escoto Brockman alipotoa risala kwenye ufunguzi wa mkutano, alisema, jamii ya kimataifa lazima ifanye mageuzi ya kimsingi kuhusu mfumo wa mambo ya fedha wa dunia, la sivyo itashindwa kurejesha imani iliyopotezwa kutokana na msukosuko wa fedha unaoenea hivi sasa duniani. Alisema, jamii ya kimataifa inawajibika, vilevile ina nafasi ya kujadili mkakati wa muda mrefu zaidi, wala siyo kujadili namna ya kulinda benki, kutuliza masoko ya utoaji wa mikopo na kuhakikisha uwekezaji, kwani yote hayo ni hatua zinazochuliwa kwa hivi sasa tu.

Bw. Brockman alisisitiza, mfumo wa hivi sasa wa mambo ya fedha duniani hauoneshi utandawazi wa uchumi wa dunia wala hali ya kutegemeana kwa uchumi wa dunia. Utatuzi wa msukosuko wa fedha wa sasa ni kujenga mfumo mpya unaoshirikisha nchi zote kwa njia ya demokrasia.

Mtaalamu mkuu wa uchumi wa Benki ya Dunia, aliyewahi kupewa tuzo ya Nobel, Bw. Joseph Stiglitz anaunga mkono msimamo wa Bw. Brockman, anasema, sasa ni "wakati wa kujenga "mfumo mwingine wa misitu ya Bretton". Alisisitiza kuwa, hakuna budi kufuata kanuni 4 wakati wa kukabiliana na msukosuko huo wa fedha, yaani kuhakikisha kuwa na haki na umoja wa jamii, umoja na ushirikiano wa jamii ya kimataifa, ulingano wa lazima kati ya serikali na masoko, na demokrasia na uwazi katika mchakato wa ujengaji wa utaratibu.

Alipotoa hotuba, Bw. Stiglitz alikosoa makosa yaliyofanywa na Marekani pamoja na baadhi ya serikali za nchi nyingine, alisema, "zilizifanya benki zao zijipanue kupita kiasi, hatimaye kufikia hali ya kulazimika kuzisaidia na kutoweza kuziacha zifilisike", sasa dunia nzima inatakiwa kukabiliana na matokeo hayo yaliyosababishwa na makosa yao. Alisema, ingawa nchi mbalimbali zimechukua hatua za kila aina kuokoa sekta ya benki na mfumo wake wa fedha, lakini watu wale waliopoteza nyumba na ajira, hawajaweza kupata fidia wanayostahili.

Bw. Stiglitz alisema, hakuna uhusiano mkubwa kati ya masoko yaliyostawi hivi karibuni na makosa yaliyosababisha msukosuko huo wa fedha, lakini yote yanakumbwa na msukosuko, hivyo, njia yoyote ya utatuzi ya kimataifa lazima isisahau nchi hizo. Alishauri kuwa, katika siku za baadaye ubunifu wa sera za mfumo wa fedha wa dunia, lazima ufanywe katika muundo wa kimataifa wa kisiasa unaowakilisha nchi mbalimbali, ambapo nchi zenye pato la wastani na zilizoko nyuma kimaendeleo, zinaweza kutoa sauti yao, alisema, Umoja wa Mataifa ndio muundo wa aina hiyo.

Washiriki wa mkutano walieleza maoni yao kuhusu mageuzi ya mfumo wa fedha wa kimataifa na kuanzisha ushirikiano wa nchi nyingi. Mjumbe wa Ufaransa aliyetoa hotuba kwa niaba ya Umoja wa Ulaya, alisema, nchi zote zinatakiwa kuzingatia namna ya kujenga mfumo mpya wa usimamizi wa kimataifa, ili kila nchi iliyoathirika iwe na haki ya kushiriki na kubeba jukumu.

Mjumbe wa Antigua na Burbuda alipotoa hotuba kwa niaba ya kundi la nchi 77 na China alisema, nchi zote wakati zinapofuatilia utatuzi wa msukosuko wa fedha, zinatakiwa pia kuzingatia namna ya kunasua uchumi wa dunia.

Washiriki wa mkutano wamesema wataalamu wa maendeleo na uchumi wa dunia, siyo wale kutoka vyuo vikuu vichache maarufu vya duniani, bali walikuwepo wale kutoka kila sehemu ya dunia zikiwemo China, India, Mexico, Korea ya kusini, Brazil na Algentina.