Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-11-03 16:03:31    
Utamaduni wa dini ya Kibuddha katika Mlima E Mei na Mlima Leshan

cri

Katika kipindi hiki maalum cha chemsha bongo kuhusu "Vivutio vya Mkoa wa Sichuan", leo tunawaletea makala ya tatu kuhusu utamaduni wa dini ya kibuddha. Kwanza tunatoa maswali mawili. La kwanza, Je Mlima E Mei ni moja kati ya sehemu takatifu za dini ya kibuddha nchini China? La pili, Sanamu ya Buddha mkuu ya Leshan ni sanamu kubwa kabisa duniani, je, urefu wake ni mita ngapi?

Mlima Emei unasifiwa kuwa ni "Mlima wa kwanza wa China". Inasemekana kuwa mapema ya karne ya 4, mtawa mmoja wa India aitwaye Bao Zhang baada ya kutembelea Mlima E mei, alishangazwa na vivutio vya mlima huo na kuusifu kuwa ni Mlima wa kwanza katika Zhendan, maana ya Zhendan ni mahali jua linapochomoza, ni jina la heshima lililotolewa na India kwa China. Tangu hapo Mlima E mei ulijulikana duniani kwa sifa yake ya "Mlima wa kwanza wa China".

Miongoni mwa milima maarufu nchini China, Mlima E mei ni wenye mwinuko mkubwa zaidi wenye mita 3000 kutoka usawa wa bahari. Na ni tofauti kuwa kwenye hali joto ya kilele cha mlima na ile ya chini ya mlima, hali hiyo imeweka mazingira mazuri kwa ukuaji wa mimea ya aina tofauti. Takwimu zilizokusanywa zimeonesha kuwa kwenye Mlima Emei, kuna zaidi ya aina 5000 za mimea, ambazo ni sawa na zile za jumla za mimea ya Bara la Ulaya, miongoni mwa mimea hiyo, pia kuna aina kadha wa kadha za mimea yenye thamani kubwa ambazo ni nadra kuonekana katika sehemu duniani.

Watalii wakitembea kwenye sehemu ya milimani, kando mbili za njia kuna miti mingi za kale, popote walipokwenda wanaweza kuona rangi ya majani ya miti na mimea. Kutokana na mabadiliko ya majira na tofauti ya hali ya kijiografia ya milima, pamoja na vivutio vya hali tofauti ya hewa, Mlima E mei unaonekana na sura za aina mbalimbali zinazopendeza. Kwa kweli kutokana na jina lake, E mei, maana yake ya kichina ni nyusi za msichana, mithili hii imeonesha vilivyo sura inayopendeza ya Mlima Emei.

Hali pekee ya utakatifu ya Mlima Emei inahusiana sana na utamaduni wa dini ya Kibuddha unaoonekana katika sehemu ya mlima huo. Mapema katika karne ya kwanza, Dini ya Kibuddha ya India ilienea kwenye Mlima E mei, ambapo hekalu la kwanza la dini ya kibuddha la China lilijengwa huko. Baadaye mahekalu mengine yalijengwa moja baada ya jingine pembezoni mwake, siku nenda siku rudi Mlima E mei ukawa moja kati ya sehemu takatifu za dini ya Kibuddha nchini China, ambapo waumini wa dini hiyo wanakwenda huko kuhiji bila kusita.

Kwenye Mlima Emei anaabudiwa Buddha Samantabhadra. Buddha Samantabhadra ni mtoto wa kwanza wa mabuddha wote duniani, katika kila sehemu yenye Buddha, hakika anakuwepo Buddha Samantabhadra. Hivi sasa katika Mlima E mei, kuna watawa 300 hivi, na mahekalu karibu 30.

Watalii wakitembea kwenye Mlima Emei, huwa wanaweza kuingia kwenye hekalu, ambalo lina historia ndefu na hali isiyofahamika. Huenda wanaweza kuona shughuli za kidini zinazofanyika kwenye hekalu, ambapo watawa na waumini wa dini wanafanya shughuli za kidini katika ukumbi wa hekalu wa kuabudu Buddha.

Kilele cha dhahabu ni kilele cha juu kabisa cha Mlima E mei, kilele hicho kinawavutia zaidi watalii. Kwenye sehemu ya kilele hicho, mbali na mahekalu makubwa matatu yenye rangi ya dhahabu, Sanamu ya rangi ya dhahabu ya Buddha Samantabhadra yenye urefu wa mita 48 inavutia sana watu. Mwongozaji wa watalii Bibi Yang Tao alimwambia mwandishi wetu habari akisema:

Sanamu hiyo inaonesha kuwa Buddha Samantabhadra ameshika kinyago cha Ruyi, maana yake ya kichina ni baraka, na kuvaa kofia ya dhahabu, sanamu ya Buddha huyo inaonekana kuwa na sura makini, Buddha amekaa juu ya mgongo wa ndovu mwenye meno 6, na sura ya Buddha inaonekana na hisia za binadamu za hisia za furaha, hasira, na huzuni, na watu wanaokaa upande wowote wanaweza kuona sura ya mbele ya Buddha Samantabhadra ambaye anawaangalia raia wote na kuwaletea heri na baraka.

Bwana Lee Geun Won ni mwamini mtiifu wa dini ya Kibuddha, safari hii alifunga safari kutoka Korea ya kusini na kufika Mlima E mei kuabudu Buddha Samantabhadra, alisema:

Safari hii nimefika Mlima E mei na kuona sanamu kubwa namna hii ya Buddha Samantabhadra, kweli naona China ni nchi kubwa yenye utukufu. Nimesujudu mara 10 mbele ya sanamu ya Buddha, na pia nimesujudu mara 3 kwenye ukumbi wa kuabudu Buddha Samantabhadra, tena nimetoa mchango kwa hekalu hilo, ingawa sikutoa hela nyingi, lakini hii imeonesha nia yangu ya dhati.

Mbali na kuwa mahali pa kuabudu Buddha, Kilele cha dhahabu pia ni mahali pazuri kabisa pa kutazama jua linavyochomoza kutoka mashariki, na kutazama bahari ya mawingu. Watalii wakisimama kwenye Kilele cha dhahabu wanaweza kuona kuwa kila jua likichomoza kutoka mashariki, mbingu huwa wa rangi ya kimanjano kabisa, ambapo milima na sehemu nzima zinamulikwa na mwangaza wa rangi ya dhahabu, mandhari ya sehemu hiyo ya wakati huo inapendeza sana; baada ya jua kuchomoza, ukungu unatoweka milimani, na mawingu meupe yanaelea juu kutoka chini ya milima, ambapo mawingu yanakusanyika pamoja mithili ya bahari kubwa ambayo inaenea zaidi mpaka kwenye mbingu isiyo na kikomo, mandhari ya sehemu hiyo ya wakati huo pia inawashangaza sana watu.

Kama watalii wakipata bahari nzuri, wanaweza kutazama hali ya mwuujiza, kwa dini ya Kibuddha, tunasema wanaweza kuona "Mwanga wa Buddha". "Mwanga wa Buddha" ni hali moja ya fizikia ya kimaumbile iliyo ya umaalum sana, ambayo inaonekana kama ni duara moja lenye rangi 7, na kivuli cha mtu kitakuwa katikati ya duara, kwa kufuata vitendo vya mtu, ndani ya duara inaweza kutokea mabadiliko mbalimbali yanayowashangaza watu. Lakini kutokea kwa "Mwanga wa Buddha" kunatakiwa chini ya makutano ya mwangaza wa jua na hali ya sura ya ardhi.

Dini ya Kibuddha imechangia utamaduni wa Mlima wa E mei katika mchakato wa maendeleo ya Mlima E mei, hasa mahekalu mengi na sanamu za Buddha, hayo yote yamekuwa utamaduni wa jadi wa Mlima wa E mei unaopatana na mandhari nzuri ya mlima huo. Kutokana na hayo, Shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO liliuweka Mlima E mei kwenye orodha ya mali ya urithi wa kimaumbile na utamaduni duniani.

Baada ya kutembelea Mlima E mei, watalii wanaweza kufunga safari kwenda Sehemu ya Leshan iliyoko kwenye umbali wa kilomita 30 magharibi ya Mlima E mei, ambapo wataona Sanamu kubwa ya Buddha ambayo ni sanamu kubwa kabisa duniani, wakiona sanamu hiyo hakika watashangaa na kuvutiwa na utiifu wa waumini wa zama za kale kwa dini ya Kibuddha.

Sanamu hiyo ya Buddha Maitreya ilichongwa kwenye mlima. Kimo cha sanamu ni zaidi ya mita 70, upana wa mabega ya Buddha ni zaidi ya mita 20, kichwa cha sanamu kiko sawa na kimo cha mlima, na miguu ya sanamu ipo kwenye kando ya mto, na mikono ya sanamu ya Buddha inashikilia kwenye magoti, sura ya sanamu ya Buddha inaonekana ya utulivu, baadhi ya watu waliwahi kusema Mlima huo ni mithili ya Buddha, na Buddha ni mithili ya mlima huo. Basi, je, ni kwanini watu walijenga sanamu kubwa namna hii ya Buddha, na ni nani waliijenga? Mwongozaji wa watalii Bibi Wu Liping alisimulia hadithi moja akisema:

Sanamu hiyo kubwa ya Buddha ya Leshan ilianza kujengwa katika Enzi ya Tang, awali aliyechonga sanamu hiyo alikuwa mtawa mmoja aitwaye Haitong aliyetembelea mkoa wa Sichuan, ambapo aligundua kuwa Mlima Leshan uko kwenye sehemu ya makutano ya mito mitatu, ajali za meli zilitokea mara kwa mara katika sehemu hiyo, hivyo akaamua kuchonga sanamu kubwa ya Buddha ili Buddha aweze kuwabariki wakazi wa huko Leshan na kutokomeza ajali mitoni. Mtawa huyo akachangisha fedha katika sehemu mbalimbali nchini China, baadaye alirudi sehemu ya Lesha, lakini aliombwa rushwa na ofisa mmoja wa ufisadi, mtawa huyo alikasirika sana, alisema naweza kujitoa macho yangu, lakini siwezi kutoa mali za Buddha, halafu alijitoa macho yake mawili, ofisa huyo aliogopa sana na kukimbia haraka. Lakini wakati uchongaji wa kichwa cha sanamu ya Buddha ulipokamilika, mtawa Haitong alifariki dunia.

Baadaye watu wa vizazi viwili walifanya juhudi kubwa kwa miaka 90 hivi, uchongaji wa Sanamu kubwa ya Buddha ya Leshan ukakamilika kabisa. Hata hivi leo watalii wakitazama sanamu hiyo kubwa ya Buddha kutoka mbali, pia wanaweza kushangaa na kusifu ustadi murua waliokuwa nao wachongaji wa sanamu na kusifu moyo wa kujitolea ya mtawa Haitong. Ndio maana waumini wengi wa dini ya Kibuddha wanafika Mlima Leshan kuabudu sanamu ya Buddha. Buddha hai Norbu Rinpoche wa Hekalu la Dongnala la Mkoa wa Qinghai, magharibi ya China ni mmoja kati yao, alisema:

Kwa sisi waumini wote wa dini ya Kibuddha, tunaweza kufika hapa na kuabudu Sanamu kubwa ya Buddha mkuu yenye historia ndefu na sura inayotulia, kweli tunaona moyo wetu umetakaswa, na kupata mwamko mkubwa sana.

Wasikilizaji wapendwa, Mlima E mei, mandhari nzuri ya maumbile ya Mlima Leshan, na utamaduni wa kidini ya sehemu hizo wenye historia ndefu, yote hayo yanastahili kusifiwa.

Sasa tunarudia maswali mawili. La kwanza, Je Mlima E Mei ni moja kati ya sehemu takatifu za dini ya kibuddha nchini China? La pili, Sanamu ya Buddha mkuu ya Leshan ni sanamu kubwa kabisa duniani, je, urefu wake ni mita ngapi?

Tunaamini kuwa baada ya kusikiliza matangazo yetu ya makala hii hakika mmepata majibu ya maswali hayo. Na matangazo ya makala hii ya tatu ya chemsha bongo yatarudiwa katika kipindi cha sanduku la barua .