Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-11-07 16:15:20    
Eneo la viwanda la Suzhou lajenga eneo jipya la kisasa

cri

Eneo la viwanda la Suzhou lililoko mashariki mwa mkoa wa Jiangsu ni eneo la aina mpya la vielelezo vya ustawishaji wa viwanda. Ukienda eneo hilo utagundua kuwa katika eneo hilo si kama tu kuna vituo vya viwanda vya teknolojia mpya za hali ya juu, bali pia kuna jumba la opera na majengo ya nyumba za wakazi. Eneo hilo linaonekana kuwa ni eneo jipya mji wa Suzhou badala ya eneo la viwanda. Serikali ya mji wa Suzhou imetunga mpango kuendeleza eneo hilo kuwa eneo la kisasa la mji huo.

Mwezi Mei mwaka 1994, eneo la viwanda la Suzhou ambalo ni mradi wa ushirikiano kati ya serikali za China na Singapore ulianza kujengwa kusini mwa mji wa Suzhou. Katika miaka 14 iliyopita, eneo hilo lilikuwa limepata maendeleo mazuri ya haraka. Ongezeko la viwango muhimu vya kiuchumi vya eneo hilo kwa mwaka lilikuwa zaidi ya asilimia 30, vitega uchumi vya nje vyenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 14.7 vimetumiwa, na eneo hilo limeleta nafasi laki 5.1 za ajira. Thamani ya uzalishaji mali wa eneo hilo katika mwaka 2007 ilikuwa zaidi ya yuan bilioni 80, ambayo iliongezeka kwa mara 100 kuliko ile ya wakati eneo hilo lilipoanzishwa. Na mitaji kutoka nchi za nje iliyotumiwa kwenye eneo hilo ilikuwa zaidi ya dola za kimarekani bilioni 1.5 katika miaka minne iliyopita. Kwa ujumla maendeleo ya eneo hilo yanachukua nafasi ya pili kati ya maeneo ya ustawishaji wa viwanda ya ngazi ya kitaifa nchini China. Katibu wa kamati ya mji wa Suzhou Bw. Wang Rong alisema kufanya uvumbuzi kwenye msingi wa kujifunza uzoefu wa sehemu nyingine ni sababu ya mafanikio ya eneo la viwanda la Suzhou, akisema,

"Eneo la viwanda la Suzhou kweli ni mradi mkubwa zaidi wa ushirikiano na mradi unaopata mafanikio makubwa zaidi kati ya China na Singapore. Eneo hilo ni moja kati ya maeneo ya ustawishaji wa viwanda yanayopata maendeleo makubwa zaidi duniani. Ni lazima eneo la viwanda la Suzhou litangulie kujifunza uzoefu wa sehemu nyingine, na kufanya uvumbuzi kwenye msingi wa kujifunza uzoefu, basi litaweza kuwa mfano mzuri wa kuigwa."

Hivi sasa katika eneo la viwanda la Suzhou kuna makampuni 77 ambayo ni miongoni mwa makampuni 500 yenye nguvu kubwa zaidi duniani, makampuni ya kigeni zaidi ya 3000, na vituo 9 vya uvumbuzi vya ngazi ya kitaifa. Eneo hilo pia limetangulia kujenga eneo la vielelezo vya viwanda linalohifadhi mazingira ya asili nchini China.

Katibu wa kamati ya eneo la viwanda la Suzhou Bw. Ma Minglong alisema eneo hilo limebuni wazo la kuwavutia wafanyabiashara, kunufaisha wakazi na kuhifadhi mazingira, akisema,

"Uzoefu wa Singapore umeonesha wazo la kisasa la uendeshaji wa maeneo ya viwanda duniani. Uzoefu wao unatusaidia sana. Kwa ukweli tumefanya uvumbuzi mkubwa kwenye msingi wa kujifunza uzoefu wao, siyo kuiga moja kwa moja mfano wa sehemu nyingine tu. Katika miaka 14 iliyopita tulitekeleza wazo la kuwavutia wafanyabiashara, kunufaisha wakazi na kuhifadhi mazingira."

Ingawa kuwavutia wafanyabiashara si uvumbuzi wa eneo la viwanda la Suzhou, lakini kumekuwa kiini cha wazo la maendeleo la eneo hilo. Aidha, ili kutoa huduma bora katika mambo yote na wakati wote, idara mbalimbali za kamati ya usimamizi wa eneo hilo zinashughulikia mambo ya kiuchumi na kijamii kwa mujibu wa sheria, na kuanzisha mazingira mazuri ya ushindani yenye uwazi, usawa na haki. Kutokana na hatua hizo, eneo la viwanda la Suzhou limekuwa eneo zuri la kufanya uwekezaji na kuanzisha shughuli.

Bw. Zhang Peizhuo ni mtaalamu wa sayansi na teknolojia anayefanya kazi katika eneo la viwanda la Suzhou. Ana uzoefu wa kushughulikia utafiti wa kemikali ya nucleic acid na utengenezaji wa bidhaa husika kwa miaka 15, na amepata hakimiliki tatu za ubunifu. Mwanzoni alianzisha kampuni ya utengenezaji wa dawa mjini Shanghai. Hivi sasa ameanzisha kampuni yake kwenye eneo la viwanda la Suzhou, na kushughulikia utengenezaji wa aina mpya za dawa. Bidhaa moja ya kampuni yake imechukua asilimia 50 ya soko la China, na imeanza kuingia soko la kimataifa. Bw. Zhang alisema,

"Baada ya kuanzisha kampuni yetu katika eneo la viwanda la Suzhou, kazi za kampuni yetu zinaendelea hatua kwa hatua kwa mujibu wa mpango uliowekwa. Mazingira ya eneo hilo ni mazuri zaidi duniani. Nafikiri tulifanya uchaguo sahihi sana."

Jambo linalolifanya eneo la viwanda la Suzhou liwe la fahari kubwa zaidi si kuzalisha yuan milioni 100 kwa siku wala kuvutia vitega uchumi vya dola za kimarekani milioni 4 kwa siku, bali ni kuhakikisha maji na hewa iwe safi baada ya kuanzishwa kwa viwanda kwa miaka 10.

Katika miaka mingi iliyopita, eneo la viwanda la Suzhou linatilia maanani uhifadhi wa mazingira, na kusimamia uhifadhi wa mazingira kwa makini. Eneo hilo limechukua hatua mbalimbali zikiwemo kutoruhusu miradi ambayo itasababisha uchafu usioweza kuondolewa kujengwa kwenye eneo hilo, kujenga miradi ambayo utoaji wa uchafu wao unaweza kudhibitiwa, kudhibiti kwa makini umbali kati ya eneo la viwanda na majengo ya nyumba za wakazi, na kushughulikia takataka kwa pamoja.

Hadi hivi sasa kwa ujumla miradi zaidi ya 200 hairuhusiwi kujengwa kwenye eneo la viwanda la Suzhou kutokana na uhifadhi wa mazingira. Eneo hilo pia limetangulia kufanya majaribio ya kuendeleza uchumi wa mzunguko na kujenga eneo la viwanda linalohifadhi mazingira ya asili. Mwezi Mei mwaka huu eneo hilo lilisifiwa kuwa ni "eneo la vielelezo vya viwanda la kitaifa linalohifadhi mazingira ya asili". Naibu mkurugenzi wa idara ya uhifadhi wa mazingira wa eneo hilo Bi. Wang Xuejun alisema,

"Mwezi Oktoba mwaka huu, tutaanzisha shughuli ya wasimamizi wanaojitolea wa uhifadhi wa mzingira, ili wakazi waweze kutusaidia kusimamia uhifadhi wa mazingira katika eneo hilo. Pia tutaanzisha shirikisho la mazingira, afya na usalama."

Ofisa mhusika wa eneo la viwanda la Suzhou alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, katika miaka 14 iliyopita eneo hilo limepata mafaniko kadha wa kadha katika ustawishaji wa viwanda, na hivi sasa litaendeleza shughuli za utengenezaji na huduma za kisasa kwa pamoja. Kwa mujibu wa mpango wa mji wa Suzhou, eneo hilo litakuwa eneo kuu la kibiashara la mji huo.