Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-11-05 20:58:15    
"Kiu ya kutaka mageuzi" yamsaidia Obama kushinda uchaguzi mkuu kirahisi

cri

Kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyotangazwa na vyombo vya habari nchini Marekani, mgombea wa Chama cha Demokratic ambaye ni seneta wa jimbo la Ilinois Bw. Obama tarehe 4 ameshinda uchaguzi mkuu, na atakuwa rais wa 56 wa Marekani. Wachambuzi wanaona kuwa kushinda uchaguzi huo kirahisi kwa Bw. Obama kumeonesha kwa mara nyingine kwamba kutaka mageuzi ni nia ya Marekani.

Bw. Obama alizaliwa mwaka 1961 huko Honolulu Hawaii, baba yake alikuwa ni mwanafunzi wa Kenya aliyesoma nchini Marekani na mama yake ni mtu mweupe . Kwa hiyo Bw. Obama atakuwa rais wa kwanza mwenye asili ya Afrika, katika historia ya Marekani, na ataapishwa tarehe 20 Januari mwaka kesho. Hivi sasa mgombea wa urais aliyetoka Chama cha Rupablican Bw. McCain amekubali matokeo ya uchaguzi kuwa ameshindwa na kumpigia simu ya kumpongeza, huku anataka wafuasi wake wamwunge mkono Bw. Obama ili kuondoa hitilafu na kuhakikisha utulivu na ustawi wa taifa. Rais wa sasa Bw. Bush pia alimwalika Bw. Obama atembelee ikulu.

Wachambuzi wanaona kuwa kushinda uchaguzi mkuu kirahisi kwa Bw. Obama kumethibitisha kwa mara nyingine nguvu ya kutaka mageuzi nchini Marekani, watu waliompigia kura Bw. Obama walisema Marekani inatakiwa mabadiliko, na wao wanapenda kuwa ni sehemu ya mabadiliko hayo.

Marekani ya hivi leo imezama katika hali ya taabu katika mambo ya ndani na nje, hasa msukosuko wa fedha unaoikumba nchi hiyo umempatia Obama msingi imara wa kupata ushindi katika uchaguzi huo. Msukosuko wa fedha ulioanzia Marekani umeenea hadi dunia nzima, mfumo wa uchumi wa kibepari uliotekelezwa na rais Bush unakosolewa. Wakati huo Bw. Obama bila kupoteza fursa ameshika suala hilo kujipatia kura. Anatetea kufuata kimsingi sera za Chama cha Demokratic, kupanua uwezo wa serikali wa kuingilia mambo ya uchumi, na kupunguza tofauti kati ya matajiri na watu maskini na kuleta ustawi wa pamoja. Zaidi ya hayo ametangaza mpango wake wa kuokoa msukosuko wa fedha. Lakini Bw. McCain alishindwa kutoa mkakati wake ulioaminika wa kuokoa uchumi akiwakatisha moyo watu wa Marekani waliokumbwa na msukosuko wa fedha.

Kuhusu sera za diplomasia, kutokana na vita dhidi ya Iraq, watu wa Marekani wanalalamika sana. Lakini Bw. Obama ameahidi kwamba kama atashinda uchaguzi mkuu ataondoa jeshi la Marekani kutoka Iraq ndani ya miezi 16 tokea ashike urais na huku akiahidi kuongeza askari 7000 nchini Afghanistan kushikilia mapambano dhidi ya ugaidi. Zaidi ya hayo pia amesema kwamba atafanya mazungumzo na viongozi wa Iran, Syria, Korea ya Kaskazini na Venezuela. Sera zake hizo za kulinda maslahi ya Marekani na zenye unyumbufu zinakubaliwa na wamarekani.

Bw. Obama ni kijana, ambaye alizaliwa katika familia ya raia wa kawaida, na ni mwenye asili ya Afrika, hayo yote yalimsaidia kupata ushindi katika uchaguzi wa rais. Wapiga kura walisema, kwa juhudi zake mwenyewe amepata mafanikio yasiyo ya kawaida.

Mabadiliko ya muundo wa wapiga kura pia yalimsaidia Bw. Obama. Habari zilizotolewa kuhusu uchaguzi zinasema wahamiaji nchini Marekani na wapiga kura vijana wameongezeka kwa kiasi kikubwa, na Bw. Obama ana ushawishi mkubwa kwa watu hao. Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni ya raia, Bw. Obama anaungwa mkono na wapiga kura wengi wanawake, wenye asili ya Afrika na Hispania na vijana wengi.

Wachambuzi wanaona kuwa ingawa Bw. Obama ameshinda uchaguzi mkuu, lakini kweli ataweza kutimiza ahadi zake kama alivyosema? Kwani msukosuko wa fedha haukutokea ghafla bali ni matokeo ya miaka mingi, sera za kiuchumi za Obama zinaweza kuleta ufanisi kama anavyotarajia? Aidha, Bw. Obama hana uzoefu wa kidiplomasia, uwezo wake wa kushughulikia mambo ya nje utathibitishwa. Wamerekani wengi wamempigia kura kutokana na ahadi zake, kama atashindwa kutimiza ahadi hizo atawavunja moyo.