Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-11-06 16:32:42    
Watu wa fani mbalimbali nchini China wamkumbuka mwongozaji mkubwa wa filamu Bw. Xie Jin

cri

Hivi karibuni mwongozaji mkubwa wa filamu wa China Bw. Xie Jin amefariki dunia kutokana na ugonjwa akiwa na umri wa miaka 85. Siku hizi watu wa fani mbalimbli nchini China kwa namna moja au nyingine wanafanya maombolezo ya kumkumbuka mwongozaji huyo wa filamu aliyetoa mchango mkubwa katika mambo ya filamu.

Bw. Xie Jin alizaliwa mwaka 1923 katika ukoo wa wasomi mkoani Zhejiang, mashariki mwa China. Mwaka 1941 alijiunga na shule ya uigizaji mkoani Sichuan, na mwaka 1948 alianza kuwa mwongozaji wa filamu. Mwaka 1957 filamu aliyoongoza iitwayo "Mchezaji wa Namba 5 wa Timu ya Wanawake ya Mpira wa Kikapu" ilimpatia umaarufu mkubwa. Filamu hiyo inavutia kwa hadithi yake, na waigizaji wote ni warembo na wenye hamasa ya kujishupaza. Filamu hiyo kwa mara nyingi ilipata tuzo ya kimataifa, hadi leo filamu hiyo bado ni nzuri iliyokubalika kati ya filamu za michezo. Mwigizaji Bi. Qin Jian mpaka leo anaendelea kuihifadhi picha aliyopiga pamoja na Xie Jin wakati filamu hiyo ilipopigwa. Alipokumbusha jinsi alivyoshiriki katika uigizaji wa filamu hiyo alisema,

"Mwongozaji wa filamu Xie Jin anafanya kazi kwa makini sana, hakuchelewa kujibu barua yangu, akisema waigizaji wote wamekusanyika ila mimi na kama nikikubali kushiriki katika uigizaji wa filamu hiyo ninakaribishwa."

Katika muda wa miaka 50 Bw. Xie Jin akiwa na majukumu ya kihistoria alipiga filamu nyingi kwa usanii wake wa hali ay juu, kati ya filamu hizo ni pamoja na "Kikosi cha Wanawake", "Ndugu Wawili wa Kike wa Jukwaani", "Ah, Susu la Kulea Mtoto!", "Mchungaji wa Farasi", "Kijiji cha Furong", "Vita vya Kasumba" na nyingine zaidi ya 20 ambazo zote ni maarufu katika historia ya filamu ya China. Bw. Xie Jin ni mwongozaji wa filamu aliyepata tuzo nyingi katika mashindano ya filamu ya kimataifa. Katika miaka ya 80 na 90 ya karne iliyopita, nchi za Ufaransa, Marekani na India zilifanya maonesho ya filamu zake, wahakiki filamu walimsifu kuwa ni "mtu mwenye heshima kubwa katika nyanja ya filamu nchini China", na wahakiki filamu wa China wanaona kuwa filamu zake zinajaa utu, upendo na moyo wa ubinadamu, na zina maana za kina.

Bwana Rao Shuguang anayefanya kazi katika Jumba la Kumbukumbu za Filamu alisema,

"Bwana Xie Jin ana hadhi muhimu katika historia ya filamu ya China, ni msanii mkubwa na amerekodi historia ya miongo kadhaa ya China kwa filamu zake. Kwa sababu filamu zake zinaweza kugusa hisia za watazamaji, filamu zake zinachukua nafasi muhimu katika historia ya maendelo ya filamu nchini China."

Bw. Xie Jin alishikilia msimamo wa kuonesha hali halisi, na alisawiri wahusika kwa makini. Filamu za "Mchungaji wa Farasi" na "Kijiji cha Furong" zilionesha mapenzi matamu na utu bora katika miaka yenye misukosuko ya kisiasa nchini China, na hii ndio sababu ya kimsingi kwa nini filamu zake zinawavutia sana watazamaji wa nyakati tofauti katika muda wa miaka 50 iliyopita. Bw. Xie Jin alipokuwa hai alisema,

"Sanaa na maisha ya binadamu ni kitu kimoja, filamu nilizopiga lazima kwanza ziwe zinaweza kunisisimua. Tuzo ya kombe la dhahabu au la fedha siijali, ninachojali ni maoni ya watazamaji. Ubora wa filamu fulani hauamuliwi na mhakiki fulani, bali ni maoni ya watazamaji."

Bw. Xie Jin alikuwa ni mwalimu na rafiki aliyependwa na watu wengi. Ingawa alikuwa na tabia makini ya kimaisha lakini pia alikuwa mtu asiyejali mambo madogo madogo. Alipendelea kuvaa miwani yenye fremu pana na kupenda kuvaa kizibao chenye mifuko mingi, alipoongea alikuwa hucheka kwa sauti kubwa. Watu waliokuwa karibu naye wanafahamu kwamba yeye anapenda kunywa pombe, tena pombe kali.

Mwongozaji wa filamu Bw. Zhai Junjie ni rafiki yake wa miongo kadhaa. Kutokana na kufariki dunia kwa rafiki yake alirukwa na usingizi kwa siku nyingi. Alisema, mambo mengi aliyokuwa akifanya naye katika miongo kadhaa iliyopita yalimjia kichwani kila siku. Alisema,

"Nilikuwa rafiki yake wa miongo kadhaa. Alikuwa anakumbatia maisha na anaukumbatia umma kwa ari yake kubwa na uchangamfu wake uliowaka moyoni mwake. Alipenda kunywa pombe japokuwa asusa ilikuwa karanga kadhaa au yai moja tu. Kutokana na uhusiano wa karibu mara nyingi marafiki zake walipokunywa alinyakua glasi yao akanywa."

Mwaka 2000 alipokuwa na umri wa miaka 77 alitunga filamu ya "Mchezaji wa Namba 9 wa Timu ya Soka ya Wanawake". Hii ni filamu yake ya mwisho. Tokea hapo katika muda wa miaka minane hamu yake ya kupiga filamu haikupungua. Kila siku alikuwa anasoma soma akitafuta mada ya filamu yake.

Baada ya habari ya kifo cha Xie Jin kuenea, watu wengi waliandika makala kumwomboleza katika mtandao wa interneti, baadhi yao wanasema, Bwana Xie Jin amerekodi zama moja kwa filamu zake, wengine walisema filamu zake zimeonesha nyayo za historia."

Katika mji wa Shanghai alikoishi yalifanyika "Maonesho ya Filamu za Kumkumbuka za Xie Jin", majumba zaidi ya 20 mjini humo yalionesha filamu zake kwa wakati mmoja, huku filamu zake pia zinaoneshwa kote nchini China. Katika mji wa Beijing, mtu mmoja aliyetizama filamu yake alisema,  

"Filamu ya 'Mchungaji wa Farasi' nimetizama sasa hivi, ingawa ni filamu ya zamani lakini inanivutia kama mpya, hadithi inanisisimua. Katika miaka iliyogubikwa na hofu ya kisiasa nchini China haikuwa rahisi kupiga filamu ya mapenzi kama hiyo, ikionesha kuwa Xie Jin alikuwa na moyo wa kuwajibika kwa jamii. Yeye ni msanii mkubwa, ni msanii mkubwa wa umma."

Bw. Jiang Wen ambaye alikuwa mwigizaji mkuu katika filamu ya "Kijiji cha Furong" katika makala yake alisema "Wazazi wetu wanapenda filamu za Xie Jien, sisi tunapenda falamu zake na watoto wetu pia wanapenda filamu zake. Nilijaliwa kushiriki katika uigizaji wa filamu yake. Najipongeza maishani mwangu!"