Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-11-06 16:34:58    
Tamasha la Michezo ya Sanaa la Asia

cri

Tamasha la 10 la Sanaa la Asia lilifungwa hivi karibuni katika mji wa Kaifeng mkoani Henan, China. Kauli mbiu ya tamasha hilo ni "Upatanifu wa Asia na Kukutana kwa Furaha Mkoani Henan". Maonesho ya aina mbalimbali na shughuli nyingi za utamaduni za umma ziliufanya mkoa huo kuwa kama bahari ya furaha.

Tamasha hilo lilizinduliwa mwishoni mwa Septemba huko Zhengzhou, mji mkuu wa mkoa wa Henan. Katika muda wa siku zaidi ya kumi za tamasha hilo, wasanii karibu 2,000 wa makundi 36 ya michezo ya sanaa waliotoka nchi 22 walifanya maonesho karibu 80.

Tokea mwaka 1998 tamasha kama hilo limefanyika mara tisa katika miji ya Beijing, Hangzhou na miji mingime nchini China. Katika tamasha hilo wasanii wanatizama maonesho ya nchi nyingine huku wakiwasiliana na kufundishana. Tamasha la mwaka huu lilifanyika katika miji miwili ya Zhengzhou na Kaifeng kwa wakati mmoja. Tofauti na matamasha yaliyopita ni kwamba tamasha hilo lilishirikisha umma. Mkuu wa Idara ya Utamaduni ya Mkoa wa Henan Bi. Yang Liping alisema,

"Tofauti na matamasha yaliyopita ni kwamba tamasha hili limeshirikisha umma. Wasanii walikwenda kwenye viwanja na sehemu za makazi kuonesha michezo yao ya sanaa na huku wakiwasiliana na wakazi uso kwa uso."

Mapema kabla ya kufunguliwa kwa tamasha hilo, wito na matangazo mengi yalikuwa yametundikwa kwenye majumba makubwa na habari za maonesho ya michezo ya sanaa zilitangazwa barabarani mjini Zhengzhou, na hata magari ya taxi yalibandikwa maneno ya kuwakaribisha wageni.

Tamasha lilipofunguliwa, magari makubwa yaliyopambwa yalitembea barabarani yakichangia shamrashamra za tamasha hilo. Magari hayo yalipambwa kwa kila aina, ambapo baadhi yao yalionesha ufanisi wa michezo ya Olimpiki, na mengine yalionesha ngoma za India. Lakini kati ya magari hayo lililovutia zaidi ni gari lililopambwa kuwa ndovu wa bandia mwenye mkono mrefu ambao unapuliza maji mara kwa mara na kuwafanya watoto kando ya barabara walie kwa furaha.

Wasanii waliofuata magari hayo walikuwa karibu elfu moja, walicheza ngoma, michezo ya gonfu na kuchezesha dragoni wa bandia, watazamaji wazee walitabasamu na watoto waliruka ruka kwa furaha. Mkazi wa mji wa Zhengzhou Bi. Chen Lijia alisema,

"Nimekuja mapema kwa makusudi, shamrashamra kubwa ilioje! Hapo kabla niliweza kutizama shamrashamra hizo kwenye televisheni tu, leo hii nimeshuhudia kwa macho yangu mwenyewe. Napenda zaidi Bollywood ya India, nasubiri gari la maonesho hayo."

Baada ya kumaliza kutembelea barabarani magari hayo yalioneshwa katika uwanja wa mji huo ili watu wapige picha ya kumbukumbu. Kwa mujibu wa hesabu, katika siku kumi watu waliokwenda kutazama magari hayo walifikia milioni moja.

Kwa sababu tamasha hilo lilifanyika katika likizo ya siku ya taifa, kila siku michezo ya sanaa yenye mitindo tofauti ilioneshwa katika majumba yote mjini Zhengzhou na Kaifeng, kati ya michezo hiyo licha ya kuwepo ngoma ya India, lakini muziki wa jadi wa Japan na dansi ya kisasa ya Israel pia vilikuwepo.

Kutokana na kushangiliwa sana na watazamaji, michezo mingi ilioneshwa tena. Msanii wa Kundi la Ngoma la Bollywood Bi. Kelly Amanda alisema,

"Kwa kuona jinsi watazamaji wa China wanavyofurahia michezo yetu sisi pia tunafurahi mno, tumeonesha kwa juhudi na tumewasiliana vizuri na watazamaji."

Katika tamasha hilo mbali na michezo ya sanaa, pia zilioneshwa filamu za Asia karibu mia moja. Filamu hizo zilioneshwa katika majumba yote ya filamu, kumbi za mkutano katika vyuo vikuu, viwanja na sehemu za wakazi mijini Zhengzhou na Kaifeng.

Mwanafunzi wa chuo cha kazi za ufundi Wang Bin kwenye mlango wa ukumbi wa chuo chake alisema,

"Nafurahi sana kwa kuweza kutizama filamu nyingi za zamani na za sasa za Asia, kwa mfano, filamu ya Japani 'Manhunt' niliwahi kutizama kwenye televisheni lakini ni sehemu sehemu tu, sikuwahi kutizama filamu nzima, hii ni mara ya kwanza kutizama filamu hiyo toka mwanzo mpaka mwisho. Nataka kutizama filamu zote zitakazooneshwa katika ukumbi wetu."

Licha ya kutazama filamu, wakazi wa miji ya Zhengzhou na Kaifeng wanaweza kutembelea bustani na kushiriki shamrashamra za utamaduni zinazofanyika huko kila siku.

Katika bustani wanafunzi mia kadhaa wa shule za msingi walikuwa wakichora picha na wasanii wa kienyeji walionesha ufundi wao wa kufinyanga sanamu, kukata picha za karatasi kwa mkasi na kuchora picha kwenye gamba la yai. Fundi wa kufinyanga sanamu Bw. Liu Jinqing alisema,

"Wasanii wa nchi za nje wanacheza vizuri sana, na sisi pia tunataka kuonesha sanaa yetu ya jadi ambayo haipatikani mahali pengine ili waukumbuke mkoa wetu, nchi yetu, na baadaye huenda wakaja tena."

Kwenye ufunguzi wa tamasha hilo waziri wa utamaduni wa China Bw. Cai Wu alisema, "Maingiliano kati ya mataifa yanatokana na urafiki kati ya wananchi wa mataifa hayo."