Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-11-10 18:57:20    
Kundi la nchi 20 limefikia kwenye mwafaka kuhusu msukosuko wa fedha

cri

Mkutano mkuu wa mawaziri wa fedha na wakuu wa benki kuu za kundi la nchi 20 wa mwaka 2008, ambao ulifanyika kwa siku mbili huko Sao Paulo, Brazil, ulifungwa tarehe 9 mwezi Novemba. Mkutano huo umefikia kwenye mwafaka kuhusu kufanya ushirikiano ili kukabiliana na msukosuko wa fedha.

Katika mkutano wa siku mbili, nchi wanachana za kundi hilo zilikubali kuchukua hatua za kuongeza uwekezaji na kupunguza ushuru wa forodha ili kuepusha uzorotaji zaidi wa uchumi. Nchi hizo wanachama pia zilikubaliana kuzidi kurekebisha utaratibu wa mambo ya fedha, hususan dhidi ya shughuli za mashirika ya fedha ya hedge funds yasiyo ya benki.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika baada ya mkutano kumalizika, waziri wa fedha wa Brazil, Bw. Guido Mantega alidokeza, atatoa ratiba ya hatua kamili za kuukabili msukosuko wa fedha kati ya miezi miwili hadi mitatu baada ya mkutano wa Washinton kumalizika. Alisisitiza, viongozi wa nchi mbalimbali wanatakiwa kufanya kazi kubwa zaidi za kisiasa kuhusu maguezi ya utaratibu wa fedha wa kimataifa.

Kabla ya hapo, Ufaransa, ambayo ni nchi mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya, ilikadiria kuwa Umoja wa Ulaya unahitaji siku 100 kuchukua hatua ili kuepusha duru jipya la msukosuko wa fedha. Kuhusu hayo, Bw. Mantega alisema, atajitahidi kutoa mpango ndani ya siku 100, lakini anaona hiyo itakuwa shida kidogo kwa Marekani, kwani nchi hiyo sasa iko katika muda wa makabidhiano kati ya serikali ya awamu hii na ya ijayo.

Katika mkutano huo, Brazil ilitoa pendekezo la kufanya mageuzi kuhusu mashirika ya fedha ya kimataifa ili kuziwezesha nchi zenye masoko mapya kupata haki kubwa zaidi ya kushiriki. Bw. Mantega alisema, inapaswa kuimarisha uwezo wa kundi la nchi 20 ili kuliwezesha kuratibu vitendo vya kimataifa na kuwakilisha vizuri makundi muhimu ya uchumi duniani. Waraka wa mwisho uliotolewa baada ya mkutano huo kumalizika unasema, Shirika la Mfuko wa Fedha la Kimataifa linaweza pia kuchukuliwa kuwa ni shirika la uratibu kuhusu vitendo vya pamoja endapo baada ya mageuzi litawezesha nchi nyingi zaidi kuwa na haki ya uwakilishi.

Kwa vyovyote vile, kuimarisha uwezo wa kundi la nchi 20 na kufanya mageuzi dhidi ya mashirika ya fedha ya kimataifa kumekuwa maoni ya pamoja ya washiriki wa mkutano, Brazil vilevile ilipendekeza kupandisha ngazi ya mkutano wa kundi la nchi 20, ambao hivi sasa unashirikisha mawaziri wa fedha na wakuu wa benki kuu, kuwa mkutano wa wakuu wa nchi, ili kukuza uwezo wa kuratibu wa kundi hilo. Lakini, namna ya kufanya mageuzi haikujadiliwa kwa kina kwenye mkutano huo, kwani kubuni mpango unaoweza kukidhi maslahi ya pande mbalimbali siyo kazi inayoweza kukamilika kwenye mkutano mmoja tu, nchi zilizoendelea na nchi zenye masoko mapya zina matakwa yao tofauti, kwa hiyo, Bw. Mantega alisema, "Hayo ni majadiliano ya kiteknolojia", na "Yanahitaji muda".

Jambo linalostahili kutajwa ni kuwa China ilipongezwa na washiriki wa mkutano kutokana na hatua zilizochukuliwa nayo katika kupunguza msukosuko wa fedha duniani. Mkuu wa Benki ya Dunia kwenye mkutano na waandishi habari uliofanyika tarehe 8, alisema, serikali ya China ilifanikiwa kutumia nafasi iliyoletwa na hali nzuri ya mambo ya fedha ya kimatiafa katika miaka michache iliyopita, iliboresha miundo-mbinu kwa kutumia mitaji mingi ya nchi za nje, hizo ni "sera za busara sana".

Alisema, China ina nguvu kubwa zaidi ya kukabiliana na msukosuko wa fedha kuliko nchi yoyote nyingine kwa akiba yake kubwa ya fedha za kigeni ilizolimbikiza, na ina nguvu ya kuhakikisha kuwa uchumi wake unakuzwa kwa utulivu.

Vyombo vya habari vinasema, msukosuko wa fedha wa sasa haujaisha, kukabiliana na msukosuko huo mkubwa wa fedha kunahitaji ushirikiano mkubwa wa jamii ya kimataifa. Kundi la nchi 20 kufikia kwenye mwafaka kuhusu kukabiliana na msukosuko wa fedha, hii inanufaisha ufufuaji na utulivu wa masoko ya fedha ya kimataifa. Kama rais Luiz Inacio Lula wa Brazil alivyosema kwenye ufunguzi wa mkutano huo, hatua za upande wowote mmoja haziwezi kutatua msukosuko wa fedha wa kimataifa wa hivi sasa, isipokuwa nchi zote zishirikiane, ambapo nchi zilizoendelea zifanye kazi muhimu zaidi.