Rais mteule wa Marekani, Bw. Barack Obama tarehe 10 alasiri alikuwa na mazungumzo na rais Bush katika Ikulu, hii ni mara ya kwanza kwa rais mteule kuitembelea Ikulu. Vyombo vya habari vinasema, matembezi yaliyofanyika mara tu baada ya Bw. Obama kuchaguliwa kuwa rais yana maana ya kuonesha haraka ya kufanya makabidhiano ya madaraka ya urais.
Bw. Bush na mkewe Bi. Laura Bush waliwalaki Bw. Obama na mkewe Bi. Michelle Obama katika Ikulu kisha, Bw. Bush na mkewe waliwatembeza Bw. Obama na mkewe kwenye makazi yao mapya. Wake wa marais hao walikuwa na shughuli zao peke yao, wakati Bw. Bush na Bw. Obama walikuwa na mazungumzo kwenye ofisi ya rais kuhusu baadhi ya masuala muhimu yakiwemo ya msukosuko wa uchumi, vita vya Iraq na Afghanistan.
Ni desturi kwa rais mteule kutembelea Ikulu baada ya uchaguzi na kabla ya kuapishwa kuchukua madaraka, lakini siyo marais wengi wateule ambao wanaitembelea Ikulu kwa haraka kama Bw. Obama, ambaye alifanya matembezi hayo katika siku ya 6 baada ya yeye kuchaguliwa kuwa rais mpya.
Ingawa marais hao walikuwa na mazungumzo katika hali ya uchangamfu, lakini walikuwa na mgongano dhahiri wa kisiasa. Vyombo vya habari vinasema, Bw. Obama atafanya marekebisho makubwa kuhusu sera za uchumi na kidiplomasia. Watu wa kundi la makabidhiano ya urais la Bw.Obama pia walisema kuwa watarekebisha baadhi ya sera za serikali ya Bush. Kiongozi wa kundi hilo, Bw. John D Podesta alisema, "hadi hivi sasa serikali ya Bush bado inatekeleza baadhi ya sera zisizosaidia maslahi ya Marekani". Dalili inaoensha kuwa tofauti za pande hizi mbili ni kama zifuatazo:
Kwanza, Obama anataka kupitisha mpango wa kuhamasisha uchumi wa Marekani, ambao unapingwa na serikali ya Bush.
Pili, katika siku ya kwanza baada ya Bw. Bush kukabidhiwa urais mwaka 2001, alirudisha "sera za kuzuia uzazi wa mpango duniani" ambazo zilitelekezwa na serikali ya Bill Clinton. Sera hizo zimeleta vizuizi na changamoto kwa jitihada ya uzazi wa majira ya dunia.
Tatu, mamlaka ya ardhi ya shirikisho la Marekani ilichukua ardhi ekari laki 3.6 katika jimbo la Utah kwa ajili ya uchimbaji wa mafuta ya petroli na gesi ya asili, jambo ambalo lilipingwa na watu wanaotaka kuhifadhi mazingira ya asili, watu wa kundi la makabidhiano ya urais la Obama vilevile wameeleza maoni yao ya namna hiyo.
Nne, kuhusu utafiti wa Stem Cells serikali ya Bush ilidhibiti sana malipo yanayotolewa na serikali kuhusu utafiti huo, baada ya Obama kukabidhiwa urais, "kundi la utafiti na wagonjwa wote wanatarajia kuona mabadiliko."
Kiongozi wa kundi la makabidhiano ya urais la Obama, Bw. Podesta alisema, rais mteule Obama ana mpango kamili wa mageuzi, serikali mpya haitafuata njia ya zamani ya serikali ya Bush. Kundi la washauri wa Obama limesema, hivi sasa wanatathimini sera zile zinazotakiwa kurekebishwa, lakini mabadiliko hayo ya sera hayatatangazwa kabla ya Obama kuunda baraza la mawaziri na kushauriana nao. Sekta ya mambo ya fedha ya Marekani pia inatarajia uteuzi wa waziri mpya wa fedha, lakini msemaji wa rais mteule Obama alisema, rais Obama hatafanya uteuzi huo katika wiki hii. Bw. John D Podesta alisema, Obama hivi sasa anafikiria kuchagua baadhi ya watu wasio wa chama cha Demokratic na chama cha Republican kuchukua wadhifa muhimu katika baraza la mawaziri. Kwa kawaida baraza jipya la mawaziri hutangazwa katika mwezi Desemba, lakini vitendo vya kundi la Obama vimeanza mapema kuliko zamani. Bw. Podesta alisema, Obama alivunja rekodi nyingi katika kipindi cha uchaguzi mkuu, hali hiyo itaendelea katika siku za baadaye.
|