Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-11-12 14:12:58    
Maendeleo ya kasi ya sayansi na teknolojia yabadilisha maisha ya watu wa China

cri

Katika muda wa miaka 30 iliyopita tangu China ianze kutekeleza sera za mageuzi na kufungua mlango kwa nje. Kiwango cha sayansi na teknolojia kimeinuka kwa kasi, na kimeathiri kila upande wa maisha ya watu.

Tuanze na chakula. Kama tunavyojua, China imefanikiwa kulisha moja ya tano ya watu duniani kwa kutumia asilimia 7 ya mashamba duniani, huo ni muujiza, unatokana moja kwa moja na teknolojia ya kisasa ya kuotesha mbegu bora na upandaji. Kwa mfano wa mpunga wa chotara uliovumbuliwa na mtaalamu mashuhuri wa kilimo wa China Bw. Yuan longping, katika muda wa miaka 30 iliyopita, teknolojia hiyo imetumika kwenye shamba lenye eneo la hekta milioni 15 nchini China na uzalishaji wa mpunga kwa kila hekta umeinuka kwa kilo 4500 kuliko zamani, ambayo imeweka msingi kwa usalama wa nafaka wa China. hivi sasa mtaalamu huyo mwenye umri wa zaidi ya miaka 70 anaendelea kufanya juhudi kuelekea malengo ya juu zaidi. Bw. Yuan longping alisema:

"shamba la majaribio la kipindi cha tatu linalenga kuzalisha mpunga kilo 5400 kila ekari, tuna matumaini ya kutimiza lengo hilo ifikapo mwaka 2010."

Mbali na hayo, kutokana na matumizi ya teknolojia nyingi za kisasa za kilimo, watu wa China wameweza kula vyakula bora wala si kushiba tu kama ilivyokuwa zamani. Hivi sasa aina mbalimbali za bidhaa za kilimo zinapatikana sokoni, mboga za majani zikiwemo matango, nyanya na matikiti maji ambazo pia zinapatikana katika majira ya baridi.

Pili, tuzungumzie usafiri. Maendeleo ya kasi ya uchumi na kuinuka kwa kiwango cha teknolojia za uhandisi kumebadilisha upya hali ya miundombinu ya usafiri wa umma katika miji ya China. katika miaka 30 iliyopita, magarimoshi ya China yalikwenda kwa kasi ya kilomita 54 kila saa tu, na ilikuwa inachukua saa 20 kusafiri kutoka Beijing hadi Shanghai, hivi sasa kila sehemu inafikika kwa mtandao wa reli, barabara na ndege, na safari kutoka Beijing hadi Shanghai inachukua 1 ya 10 ya muda uliohitajika zamani.

Aidha, chombo kipya cha usafiri wa umma, yaani magari yanayoendeshwa kwa umeme, pia kimeingia kwenye maisha ya watu wa China. hivi sasa wakazi wa miji ya Beijing, Wuhan, Tianjin na Weihai wanaweza kusafiri kwa kupanda magari hayo ya umeme yaliyosanifiwa na China yenyewe. Magari ya aina hiyo hayatumii mafuta, hivyo yanatoa uchafuzi kidogo tu. Abiria mmoja wa Beijing Bi. Su Xiumin alisema,

"nadhani kwa kupanda, magari ya umeme hayana tofauti kubwa na yale ya kawaida. Lakini magari ya aina hiyo yanatoa uchafuzi kidogo tu, kama magari mengi zaidi ya aina hiyo yatatumika, sifa ya hewa mjini Beijing itaboreka kidhahiri."

Sasa tuangalie vifaa vya matumizi. Kutoka televisheni ya kitarakimu, hadi kampyuta ya hali ya juu, kutoka kamera ya kitarakimu, simu ya mkononi hadi vifaa mbalimbali vya burudani kama vile MP3, kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, maisha ya watu wa China pia yameingia kwenye zama ya kitarakimu. Kuenea kwa teknolojia ya mtandao wa Internet kumeathiri kwa undani maendeleo ya uchumi na jamii ya China.

Kwa mujibu wa takwimu husika, hivi sasa idadi ya watumiaji wa mtandao wa Internet nchini China imezidi milioni 250, na mtandao umekuwa chombo muhimu kwa watu kupata habari, kujiburudisha na kuwasiliana na wengine. Mkazi wa Beijing Bi. Sun Wen anapenda sana kutalii, katika miaka miwili iliyopita, Bi. Sun Wen alianza kufahamu kuhusu blogi kwenye mtandao, hivi sasa kuandika kumbukumbu za utalii kwenye blog yake kumekuwa sehemu isiyokosekana katika maisha yake. Bi. Sun Wen alisema:

"hivi karibuni nilikwenda kwenye mabaki ya ukuta mkuu wa zamani ulioko kwenye mikoa ya Shanxi na Mongolia ya Ndani na kuwapiga picha wakazi wa sehemu hizo, katika safari hii niliona hali ya maisha na kazi za watu wa huko. Baada ya kurudi, niliandika kumbukumbu za maoni na hisia zangu kwenye blog yangu. Marafiki zangu hawakuweza kutembelea pamoja nami, lakini wao pia wanaweza kujua mandhari ya huko kutokana na jinsi nilivyoielezea safari kwa kupitia blog yangu."

Aidha, teknolojia za mtandao wa Internet pia zinatumika katika kuboresha huduma za serikali kuhudumia umma. Kwa mfano China ilianzisha mradi wa elimu masafa ya kisasa kwenye shule za msingi na za sekondari vijijini katika miaka minne iliyopita, mradi huo ulifanya asilimia 80 ya shule za vijijini ziwe na uwezo wa kutoa elimu masafa. Kwa kutumia mtandao wa kompyuta na televisheni za saitelaiti, watoto wa vijijini pia wanaweza kufundishwa na walimu mashuhuri walioko mbali. Mwanafunzi wa shule ya msingi ya tafara ya Huizhai mkoani Guangdong Li Xiang alisema, mbinu hiyo ya ufundishaji inamvutia sana, alisema:

"darasa la elimu masafa ni kama kutazama filamu, kuna picha za cartoon pamoja na sauti, zinavutia sana."

Lakini mabadiliko hayo yote hayakutegemewa katika miaka 30 iliyopita. Wakati huo, kutokana na upungufu mkubwa wa bidhaa, watu walikuwa wananunua vitu kwa kupangiwa, kwenye baadhi ya sehemu za vijiji hata watu hawakutatuliwa suala la chakula na nguo. Mwaka 1978 China ilianza kutekeleza sera za mageuzi na kufungua mlango kwa nje, hatua hizo zilibadilisha kabisa njia ya maendeleo ya sayansi na teknolojia za China, na kuzifanya sayansi na teknolojia zitoe mchango mkubwa zaidi katika kuboresha maisha ya watu wa China.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini China katika miaka 30 iliyopita yameoneshwa wazi kwenye michezo ya Olimpiki ya Beijing iliyofanyika miezi kadhaa iliyopita. Sayansi na teknolojia mpya zilitumika katika fani mbalimbali za michezo hiyo zikiwemo ujenzi wa viwanja vya michezo, upashanaji habari, mawasiliano, usalama wa chakula, utabiri wa hali ya hewa na ulinzi wa usalama, teknolojia hizo ziliwapa urahisi wachezaji na watalii kutoka nchi mbalimbali duniani. Waziri wa zamani wa mambo ya taifa ya Uturuki anayeshughulikia mambo ya michezo Bw. Mehmet Ali Sahin ambaye alihudhuria sherehe ya ufunguzi wa michezo ya Olimpiki ya Beijing alisema:

"niliwahi kuhudhuria sherehe ya ufunguzi wa michezo ya Olimpiki ya awamu nyingi, nadhani sherehe ya ufunguzi ya michezo ya Olimpiki ya Beijing ni nzuri kabisa kuliko awamu zote zilizopita, na pia ni ile iliyotumia vizuri kabisa teknolojia mpya na za hali ya juu."