Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-11-12 18:30:18    
Kundi la wasanii la Mkoa wa Qinghai latembelea Kenya

cri

Hivi karibuni kundi la wasanii la mkoa wa Qinghai China lilishiriki Tamasha la "Wiki ya Utamaduni" katika Chuo Kikuu cha Kenyata jijini Nairobi. Katika tamasha la wiki hiyo wasanii wa kundi hilo walifanya maonesho ya nyimbo na ngoma yenye mitindo pekee ya makabila madogomadogo ya mkoa wa Qinghai wakiwaletea watazamaji wa Kenya uhondo mkubwa wa utamaduni wa China.

Mliosikia ni wimbo wa "Mapenzi Makali ya Hua'er" ulioimbwa na kundi la wasanii la mkoa wa Qinghai. Nyimbo za aina ya Hua'er zinaenea sana mkoani Qinghai kutokana na mahadhi yake nzuri, na wasanii wa kundi hilo pia walicheza ngoma ya "Kubwaga Mapenzi kwa Msichana Mzuri" na ngoma ya kabila la Wa-tu la "Kufurahia Michipukizi ya Majani".

Tamasha la "Wiki ya Utamaduni" lilianzishwa mwaka 1992, na kila mwaka linafanyika kwa mara moja. Tamasha hilo linawapatia wanafunzi wenye hamasa na kujawa na matumaini ya siku za usoni jukwaa la kuonesha uhodari wao wa michezo ya sanaa, pia linaleta fursa nzuri ya kuhimiza maingiliano na maelewano kati ya tamaduni tofauti. Katika tamasha hilo la wiki moja, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyata waliimba nyimbo na kucheza ngoma zinazounganisha mtindo wa kisasa na wa jadi wa Afrika Mashariki.

Ngoma hii ilichezwa na wanafunzi wawili wa kiume wa Chuo Kikuu cha Kenyata, ngoma hiyo inajaa nguvu na mhemeko ikionesha jinsi wanavyokumbuka maskani yao, ala iliyosaidia ngoma ni Kayamba, ambayo ni ala ya aina pekee ya Kenya. Mkuu wa Kundi la Wasanii la Mkoa wa Qinghai Bw. Zhou Bin alisema China na Kenya zina tabia za namna moja na tabia hizo zinazofanana zimeondoa kwa kiasi kikubwa ugeni unaotokana na tatizo la lugha na tofauti ya utamaduni. Alisema,

"Mkoa wa Qinghai uko katika uwanda wa juu na Kenya hali kadhalika. Watu wa makabila yaliyoko katika nyanda za juu huwa na tabia ya ukakamavu na uimara, kwa hiyo utamaduni wao pia unafanana na hasa katika muziki na ngoma. Ingawa tuna tatizo la lugha, lakini katika ufunguzi wa 'Wiki ya Utamaduni', wasanii wetu wamejifunza ngoma nyingi za Afrika. Siku mbili zilizopita wasanii wetu na wasanii wa Kundi la Chuo Kikuu cha Kenyata walifundishana ngoma, mafundisho hayo ndio maingiliano ya kiutamaduni."

Naibu mkuu wa Chuo Kikuu cha Kenyata Bi. Olive Mugenda alisifu sana utamaduni wa China wenye aina nyingi. Alisema kauli mbiu ya Tamasha la "Wiki ya Utamaduni" la mwaka huu ni "Kuthamini utamaduni wenye aina nyingi kwa ajili ya amani na umoja wa makabila". Alisema, nchini Kenya kuna makabila 42 na nchini China kuna makabila 56, hizo ni nchi zenye makabila mengi. Nia ya "Wiki ya Utamaduni" ya mwaka huu ni kuamsha jamii ihifadhi tamaduni tofauti, watu wa makabila mbalimbali waishi pamoja kwa amani, kuondoa magombano na kutimiza umoja wa taifa kwa kupitia maonesho ya utamaduni tofauti yanayotoka kutoka makabila mbalimbali nchini Kenya na nchi za nje.

Mke wa balozi wa China nchini Kenya Bi. Cai Xiaoli kwenye ufungaji wa tamasha hilo aliwaelezea watazamaji kwa Kiingereza jinsi tamasha hilo linavyochangia maelewano na kuimarisha urafiki kati ya China na Kenya. Alisema,

"Utamaduni ni njia muhimu ya kuonesha na kueleza hisia na mtindo wa kimaisha. Nilipoanza kukanyaga ardhi nzuri ya Kenya nilishangaa kwa kuona kwamba kumbe Wakenya ni watu wanaopendeza sana, wao ni watu wachangamfu na wenye kipaji cha sanaa. Nafurahi kwamba Kwaya ya Kayamba ilialikwa kufanya maonesho ya kuimba nyimbo nchini China baada ya kutokea kwa tetemeko kubwa la ardhi huko Wenchuan mkoani Sichuan, kwa sauti yao tamu waliimba wimbo wa 'Mimi Bado ni Mchina Moyoni Mwangu', wimbo ambao wachina wengi wanajua kuuimba, ambapo walionesha upendo wao kwa watu waliokumbwa na maafa ya tetemeko la ardhi, hisia zetu zimeguswa sana na nguvu ya maingiliano hayo ya utamaduni."