Mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Bw. Zhang Yesui tarehe 13 alipotoa hotuba kwenye mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa alisema kuwa, China inapinga kuhusisha ugaidi na nchi fulani, kabila na dini, na pia inafuatilia ufufuzi wa fikra yenye msimamo mkali ya kupinga uislamu, pamoja na ufashisti mpya.
Bw. Zhang Yesui alisema, katika hali ambayo suala la utandawazi wa uchumi limekukwa suala kubwa zaidi, maisha ya nchi mbalimbali duniani yanaungana karibu, hali ambayo haikutokea hapo awali. Wakati huo huo tofauti ya makabila na ubaguzi wa kidini zimesababisha migongano mikubwa huku zikijaribu kuafikiana siku hadi siku.Alisema:
Vyanzo na maendeleo ya dini na ustaarabu vinatofautiana tu hali yao ya kutokea mapema zaidi au kuchelewa zaidi, hakuna tofauti ya kiwango cha juu au cha chini. Dini zote na ustaarabu wa aina zote ni matokeo ya akili na uwerevu wa binadamu, na zote zimetoa mchango kwa ajili ya maendeleo ya jamii ya binadamu, hivyo zote zinapaswa kuheshimiwa.
Mkutano huo uliitishwa kutokana na pendekezo la mfalme wa Saudi Arabia Abdullah, ambao ulifunguliwa tarehe 12 kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, ambapo marais, viongozi wa serikali na maofisa waandamizi wapatao zaidi ya 70 wakiwemo rais George W.Bush wa Marekani, waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown, rais Asif Ali Zardari wa Pakistan, rais Shimon Peres wa Israeli na wengineo wamehudhuria mkutano huo, ambapo wamejadili kuhusu namna ya kuhimiza mawasiliano na maelewano kati ya watu wenye dini na utamaduni tofauti, ili kusukuma mbele amani ya dunia.
Bw. Zhang amedhihirisha kuwa, China inatetea kuheshimu tofauti zilizopo sasa, na kutatua migogoro kwa njia ya amani. Migogoro hutokana na hali ya kutengana, hali ya ubaguzi na hofu hata chuki zilizosababishwa na tofauti. China siku zote inatetea kupinga siasa kali, kupinga ubaguzi na hali ya kuwatenga watu wasio wa kabila moja au wa dini moja ama kuwatenga wageni. Alisema, nchi mbalimbali zinapaswa kutilia maanani kutoa elimu kwa vijana juu ya fikra ya utamaduni wa amani. Alisema:
China inatetea kutoa elimu kwa vijana ili wawe na mitizamo sahihi kuhusu ustaarabu na dunia, vijana ni jamii ya siku za mbele za binadamu, serikali za nchi mbalimbali zinapaswa kuwajibika katika kuchukua hatua za muda mrefu zenye ufanisi za kuwafundisha mawazo ya kutendeana kwa uvumilivu, kuelewana na kuheshimiana, na kuwawezesha wawe na uwezo wa kukinga chuki za kidini na kupinga ubaguzi.
Katika hotuba yake Bw. Zhang alisisitiza zaidi umuhimu wa vyombo vya habari katika mchakato wa kuwaelimisha vijana. Alisema:
China inatetea vyombo vya habari vya nchi mbalimbali vibebe kwa hiari wajibu wa jamii, na kueneza utamaduni wa amani, kuhimiza hali ya kutendeana kwa uvumilivu, maelewano na masikilizano kwenye jamii, kutoa habari sahihi na zenye manufaa kwa umma, kulinda maadili na haki za jamii, na kukwepa kutoa maneno yanayoweza kuchochea mapambano kati ya dini na utamaduni tofauti.
Bw. Zhang alisema mwishoni kwamba, katika miaka mingi iliyopita serikali ya China inaunga mkono kithabiti na kujitahidi kushiriki katika juhudi zote za jamii ya Kimataifa kwa ajili ya kuhimiza mazungumzo kati ya nchi zenye dini na utamaduni tofauti. Ameeleza matumaini kuwa mapendekezo na taratibu husika zitaweza kusaidiana na kuwa nguvu na daraja la mawasiliano na ushirikiano katika kusukuma mbele maendeleo ya pamoja ya jamii ya binadamu, ili kutoa mchango wa kujenga dunia nzuri yenye masikilizano.
|