Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-11-14 16:06:21    
"Tamasha la Utamaduni wa Afrika Mwaka 2008" lastawisha maingiliano ya kiutamaduni kati ya China na Afrika

cri

"Tamasha la Utamaduni wa Afrika Mwaka 2008" ambalo pia ni maingiliano makubwa ya kiutamaduni kati ya China na Afrika lilifanyika mjini Shenzhen China kuanzia tarehe 23 Oktoba mpaka tarehe 2 Novemba. Wasanii na wataalamu wa Afrika na China wana matumaini kuwa China na Afrika zitaimarisha zaidi urafiki wa jadi na kukuza zaidi maingiliano hayo na kupanua maelewano kwa njia nyingi zaidi.

"Tamasha la Utamaduni wa Afrika Mwaka 2008" ni tamasha kubwa kabisa tokea mkutano wa wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika ufanyike Beijing mwaka 2006. Wasanii na wataalamu zaidi ya 140 kutoka nchi 25 za Afrika walishiriki kwenye tamasha hilo wakifanya maonesho ya utamaduni, michezo ya sanaa, maingiliano ya ana kwa ana na matembezi ya utafiti katika sehemu mbalimbali nchini China.

Moja ya shughuli za tamasha hilo ni kufanya maonesho ya utamaduni kwa pamoja, ambapo yamefanyika maonesho ya vitu vilivyohifadhiwa katika Jumba la Makumbusho la Senegal, maonesho ya sanaa ya mila na desturi za watu wa Gabon, maonesho ya vitu vya kale vilivyokopiwa vya Misri pamoja na maonesho ya picha za Afrika zilizochorwa na wachoraji wa China walipokuwa barani Afrika na machapisho ya China kuhusu Afrika. Sanaa ya Afrika inawavutia sana wasanii wa China kutokana na uzuri wake wa kiasili uliotiwa chumvi. Mwandalizi wa tamasha hilo ambaye ni naibu mkurugenzi wa Kituo cha Maonesho ya Kimataifa ya Sanaa Bw. Wan Jiyuan alisema,

"Maonesho hayo yameonesha utamaduni wa Afrika kwa ujumla na pia yameonesha utamaduni tofauti wa nchi mbalimbali barani Afrika. Sanaa ya Afrika ni ya kiasili na imejaa nguvu nyingi za uhai, wasanii wengi wa China wamefurahishwa sana wakati walipotazama sanaa ya Afrika."

Mwaka 2006 serikali ya China imeanza mpango wake wa kuwaalika waafrika wanaoshughulikia mambo ya utamaduni waje China kwa ziara. Mwaka huu mpango huo umetekelezwa na kupanuliwa zaidi, ambao umehusisha wengi wa wachoraji, wataalamu wa kutunza vitu vya kale na maofisa. Miongoni mwao wachoraji kutoka nchi tano zikiwemo Afrika Kusini, Benin, Cote d'Ivoire watakaa katika Chuo cha Uchoraji cha Shenzhen kwa miezi miwili kwa ajili ya kubadilishana taaluma za uchoraji. Mchoraji wa Kenya Bw. Edward Ndekere alipozungumza na wachoraji wa China alisema alishangaa kuona jinsi wachoraji wa China walivyo hodari katika kufanya utafiti kwa kina kuhusu utamaduni wa Afrika, kwani picha zao walizochora hazina tofauti na picha walizochora wasanii wa Afrika. Alisema,

"Wachoraji wa China wananishangaza sana, wachoraji hawa wanaielewa Afrika kwa kina zaidi kuliko Wazungu, hata picha walizochora utafikiri zilichorwa na wasanii wa Afrika."

Mkuu mtendaji wa Chuo cha Uchoraji cha Shenzhen Bi. Liu Junjie alisema chuo chake kimewapangia wachoraji walioalikwa katika shughuli za aina nyingi. Alisema,

"Wachoraji walioalikwa wanapokuwa katika chuo chetu watakuwa na shughuli za kuchora picha na kufanya maonesho ya picha zao, pia watakuwa na makongamano ya kitaaluma na kutembelea sehemu mbalimbali nchini China ili wapate fikra za kuchora picha, baadaye baadhi ya picha zao zitabaki chuoni kwetu."

Mchoraji wa Afrika Kusini Bi. Angela Banks alichora seti moja ya picha tano zikieleza alivyoiona kuhusu mageuzi ya China, maendeleo ya ujenzi wa miji na urafiki kati ya China na Afrika. Kuja kwake nchini China pia kumempatia ufahamu zaidi juu ya uchoraji wa Kichina. Alisema,

"Nilitembelea kwenye nyumba za wachoraji wa picha wa China na kuwasiliana nao uso kwa uso, kila mmoja ana urafiki mkubwa nami na wanapenda kuonesha picha zao na kutazama picha zangu, hayo ni maingiliano ya karibu sana. Baada ya kurudi nchini nitajaribu kuchora picha kwa rangi nyeupe na nyeusi kama picha za mtindo wa Kichina, nadhani nimeathiriwa na mtindo huo."

Msaidizi wa mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Kiutamaduni na Nchi za Nje katika Wizara ya Utamaduni ya China Bw. Yu Fan alieleza kwamba baada ya mkutano wa wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwaka 2006 mjini Beijing, serikali ya China ina matumaini kwamba maingiliano ya kiutamaduni kati ya China na Afrika yatakuwa ya aina nyingi, kutokana na matumaini hayo mwaka huu wataalamu wengi wa Afrika wamealikwa kushiriki tamasha hilo. Alisema,

"Kuna haja kwa idara za utamaduni kuwa na maingiliano? Na kuendeleza maingiliano hayo kwa namna gani? Ukiwa mkurugenzi wa jumba la makumbusho si unataka kufanya maonesho nchini China? Maingiliano kama hayo kati ya idara za utamaduni yatakuwa ya kina zaidi."

Mwaka huu wajumbe wa majumba ya makumbusho kutoka nchi nane wakiwa wachunguzi wamekuja China kwa nia ya kufanya utafiti na maingiliano na majumba ya makumbusho katika miji ya Beijing, Shanghai, Changchun na miji mingine. Mjumbe wa Zambia Bw. Terry Nyambe alisema jinsi Wachina wanavyothamini utamaduni wao wa jadi inawaingilia sana akilini.

"Naona Wachina wanauthamini sana utamaduni wao wa jadi, kwa mfano, ukienda kwenye kasri la ufalme mjini Beijing utaona Wachina wengi wakitazama mali zao za urithi wa utamaduni, na katika sehemu nyingine kwenye majumba ya makumbusho Wachina huwa wengi na baadhi yao wanatoka mbali. Kuenzi na kutunza utamaduni wa jadi ni jambo lenye umuhimu mkubwa."

Bw. Terry Nyambe alisema, ingawa idadi ya watu wa Zambia ni ndogo sana ikilinganishwa na idadi ya Wachina, lakini katika juhudi za kuinua mwamko wa kuthamini na kutunza utamaduni, Zambia ingepata mafanikio kama ya China. Alisema, baada ya kurudi nyumbani atahimiza juhudi hizo za idara husika.

Mwanasayansi wa Jumba la Makumbusho la Taifa la Kenya Bw. Martin Tindi anaona kuwa pande mbili zinapaswa kutembeleana na kuimarisha zaidi ushirikiano. Alisema,

"Wataalamu wa Afrika wanapokuwa China wanaweza kujionea vjiji na majumba ya makumbusho na mali nyingi za urithi wa utamaduni, kadhalika, wataalamu wa China wakiwa barani Afrika pia wanaweza kujionea mali zetu za urithi na tunaushughulikia vipi mali zao za urithi, tukae pamoja na tujadiliane. Tunaweza kuimarisha ushirikiano kwa kutembeleana kwa sababu tunayo mambo mengi ya kufundishana."

Juhudi za serikali ya China za kuwapatia wataalamu wa China na Afrika fursa ya kuzungumza ana kwa ana na kusaidiana zinasifiwa sana na maofisa wa Afrika.

Naibu waziri mkuu wa Gabon Bw. Paul Mba Abessole alipozungumza na waandishi wa habari alisema, ana furaha ya kuona mabadiliko ya maingiliano ya kiutamaduni yamekuwa ya aina nyingi, ana matumaini kuwa maingiliano hayo yatakuwa ya kina zaidi, na ya muda mrefu zaidi. Alisema:  

"Mambo yetu yameanza tu, tutaendeleza maingiliano hayo kwa kina zaidi na kuyafanya yawe ya aina nyingi zaidi na ya muda mrefu zaidi, hivyo ndivyo tunavyoweza kuhakikisha uhusiano wa pande mbili unaendelea kwa muda mrefu zaidi, imara zaidi na utulivu zaidi."