Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-11-17 17:02:00    
Yibin, Mji wa kwanza kwenye eneo la mtiririko wa mto Changjiang

cri

Wapendwa wasikilizaji, karibuni katika kipindi hiki maalumu cha chemsha bongo kuhusu "Vivutio vya mkoa wa Sichuan". Leo tunawaletea makala ya 5, tutawafahamisha kuhusu Yibin, mji wa kwanza kwenye eneo la mtiririko wa Mto Changjiang. Kabla ya kusikiliza maelezo, tunatoa maswali mawili: La kwanza, sinema ipi iliyopata tuzo ya Academy Awards, ambayo filamu yake ilipigwa kwenye msitu wa mianzi wa Shunan? La pili, Je, Mji mdogo wa kale wa Lizhuang uko kwenye kando ya Mto Changjiang? Sikilizeni maelezo ya leo kwa makini kwani majibu ya maswali hayo yamo ndani yake.

Wapendwa wasikilizaji, huenda bado mnakumbuka Sinema iitwayo "Corouching Tiger, Hidden Dragon", ambayo iliteuliwa kuwa ni sinema nzuri kabisa ya sinema za lugha za kigeni mwaka 2001 na kupewa tuzo ya Academy. Katika sinema hiyo "mapigano kwenye msitu wa mianzi" ni Sehemu inayopendeza zaidi. Mabingwa wawili wa kike na kiume wenye Wushu wa kiwango cha juu walipigana kwenye msitu huo wa mianzi, na kuonesha vilivyo sifa za Wushu wa China. Msitu wa mianzi unaoonekana kwenye sinema hiyo ni msitu wa mianzi wa Shunan ulioko kusini mashariki mwa mji wa Yibin, mkoani Sichuan, ambao unasifiwa kama moja kati ya misitu mizuri kabisa ya nchini China.

Mtu akitembea kwenye msitu wa mianzi wa Shunan wenye eneo la kilomita za mraba 120, ataona kote ni mianzi ya rangi ya kijani, maporomoko ya maji, mtiririko wa maji ya kijito na kusikia milio ya ndege, na wala hasikii joto kabisa hata kama ni katika siku za majira ya joto. Nchini China kuna shairi moja linalosema, ningekubali kukosa nyama katika chakula, nisingekubali kukosa mianzi pembezoni mwa nyumba. Mianzi inapendwa sana na watu wa China, na ni alama ya utamaduni wa China na sehemu ya mashariki ya dunia. Msitu wa mianzi wa Shunan upo kwa zaidi ya miaka elfu moja iliyopita, na ni moja ya chimbuko la utamaduni wa mianzi wa China. Mkurugenzi wa idara ya usimamizi wa sehemu ya mandhari wa bahari ya mianzi ya Shunan, Bw. Bai Hao alisema, katika sehemu hiyo si kama tu watu wanaweza kuburudishwa na utamaduni wa mianzi wa mashariki, bali pia ni mahali pazuri pa kupumzika. Alisema:

"Hapa kuna vivutio vitatu: Cha kwanza ni 'kufungua macho', sehemu hiyo ya mianzi ni ya kipekee nchini China hata katika dunia nzima, kwa kuwa na mianzi mingi ya ajabu ya aina ya Nan, hivi sasa sehemu hii imekuwa sehemu ya vivutio ya ngazi ya taifa; Cha pili ni 'kusafisha mapafu', hewa ya kwenye msitu wa mianzi ni safi na yenye negative oxygen ions nyingi, kwa hiyo ni mahali pazuri sana kwa mapumziko kwa watu na wagonjwa; Cha tatu ni 'chakula kisicho cha kawaida', ndani ya sehemu hiyo tunawaandalia wageni chakula chenye umaalumu wa utamaduni kinachoitwa 'chakula cha panda', vitu vyote vinavyotumiwa katika mapishi ya chakula vinachukuliwa kwenye msitu huo wa mianzi."

Kwenye kando mbili za njia inayopita katika mianzi ni mianzi iliyokomaa yenye rangi ya kijani iliyokoza, mianzi midogo yenye rangi ya kijani kibichi pamoja na machipukizi ya mianzi. Kutembea kwenye msitu wa mianzi, kama unabahatika huenda utaweza kuwaona sungura na ngiri, au utaweza kupata aina ya uyoga za dictyophora zinazoota karibu na mianzi.

Wageni wakifika sehemu hiyo ya mianzi huvutiwa sana na kung'ang'ania huko hata hawataki kuondoka. Mtalii kutoka Chengdu Bw. Feng Hui alisema:

"Baada ya kufika kwenye msitu wa mianzi wa Shunan, ninaona mianzi mingi ya kupendeza, nimeburudika sana, ninajisikia nimefika peponi, kweli ni mahali pazuri sana. Mbali na mianzi, hapa kuna ziwa, tunaweza kupanda mashua, pia kuna chakula kizuri sana, ninajisikia furaha na nimechangamka sana."

Sehemu nyingine inayosifiwa kama msitu wa mianzi wa Shunan ni kijiji cha Li kilichoko kwenye kiunga cha mji wa Yibin. Kijiji cha Li kiko kwenye kando ya kusini ya mto Changjiang, ni tarafa maarufu ya utamaduni yenye historia ya miaka 1,460. Hivi sasa katika tarafa hiyo bado kuna majengo mengi ya kale yanayoonesha umaalumu wa makazi ya watu wa kusini mwa mkoa wa Sichuan kati ya katikati ya karne ya 14 na mwanzoni mwa karne ya 20, ni sehemu yenye vivutio vingi, ambayo watalii hawataki kukosa kuitembelea. Jumba la kuwekea vibao vya mizimu(ancestral hall) ya mababu wa ukoo wa Zhang kwenye upande wa magharibi wa tarafa ya Li Zhuang lina eneo la karibu mita za mraba 4,000, jumba hilo lilijengwa mwaka 1840, ni moja ya majengo ya kale, ambayo yamehifadhiwa vizuri hadi hivi sasa. Jumba hilo lilijengwa kwa mbao, milango na madirisha yake ni yenye umaalumu wake.

Kila dirisha lilichongwa korongo mbili za mbao, korongo 100 za mbao zilizoko kwenye madirisha 50 zinatofautiana na zenye sura na maumbo mbalimbali, korongo hizi zinaonekana kama korongo hai. Mwongoza watalii, Bi. Zhang Hui alisema, madirisha hayo yaliyotengenezwa kwa ufundi mkubwa yana thamani kubwa sana, na yanaonesha kiwango cha juu cha ufundi wa wakati ule.

"Korongo mia zinamaanisha baraka na maisha marefu. Kumbukumbu ya ukoo wa Zhang inasema, bei ya dirisha moja ilikuwa fedha gram 700, na wakati huo, mshahara wa ofisa mmoja wa ngazi ya juu ulikuwa ni fedha gram 750."

Bi. Zhang Hui alisema, katika miaka ya 40 ya karne iliyopita,vyuo vikuu na taasisi za utafiti nyingi za China zilihamia kijiji cha Li, ambacho kilikuwa moja ya sehemu zenye shughuli nyingi za utamaduni katika kipindi cha vita vya kupambana na mashambulizi ya Japani. Wakati ule masanduku elfu kadhaa ya vitu vya kiutamaudni vya majumba ya mfalme vilivyohifadhiwa katika jumba la makumbusho yalihamishwa kwenye kijiji cha Li baada ya kupita njia ndefu, vitu hivyo vilihifadhiwa kwenye jumba hilo la ukoo wa Zhang kwa muda wa miaka 5 au 6 hivi.

Mbali na rasilimali nyingi za kimaumbile na kiutamaduni, watalii vilevile wanaweza kushuhudia mila na desturi za watu wa makabila madogo. Wilaya ya Xingwen iliyoko kusini mashariki mwa mji wa Yibin imejulikana sana na watu kutokana na kuweko mawe mengi ajabu, na inasifiwa na watu kuwa ni bustani ya jiolojia duniani. Si kama tu huko kuna mawe mengi pamoja na mapango ya mawe ya chokaa, vilevile kuna nyumba za watu wa kabila la Wamiao, zinazochukua nafasi ya kwanza mkoani Sichuan.

Kitu kingine kisicho cha kawaida ni kuwa huko ni mahali ambapo kabila moja la kale la Wabo walitoweka duniani. Mwongoza watalii wa sehemu ya mandhari ya mawe ya Wingwen, dada Yang Ting wa kabila la Wamiao, alisema, kabila la Wabo la kale lililokuweko kwenye sehemu ya kusini magharibi ya China, na lilitoweka kwenye mji wa Wang ulioko wilayani Xingwen. Kwenye sehemu ya mandhari ya mawe ya Xingwen, watu wanaweza kuona mabaki ya utamaduni wa watu wa kabila la Wabo, ambayo ni masanduku ya kuwekea maiti yaliyohifadhiwa kwa kutundikwa juu kwa juu kwenye genge la mlima. Masanduku hayo ni ya mti wa Phoebe, sasa imepita miaka mia kadhaa, lakini bado hayajaoza.

Kabila la Wabo lilitoweka katika karne ya 16, na yamebaki mambo mengi yasiyofahamika. Mbona Wabo wanaweka masanduku ya kuwekea maiti kwenye genge la mlima? Hadi hivi sasa bado kuna wasomi wanabishana. Mtaalamu wa mambo ya mila ambaye pia ni profesa wa chuo kikuu cha Sichuan, Bw. Mao Jianhua alisema, msemo mmoja ni wa kuaminiwa zaidi.

"Mazishi hayo ni tofauti na mila ya mazishi ya kawaida nchini China. Wataalamu walisema, masanduku hayo hayawekewi kwenye magenge ya kawaida ya milima, bali ni karibu na mto, walitaka mizimu yao ifuate ile ya mababu zao, kwani waliamini kuwa mababu zao walifika huko kwenye mto, hivyo walitaka mizimu yao iende kwao kabisa."

Wapendwa wasikilizaji, sasa tunarudia maswali mawali: La kwanza, sinema ipi iliyopata tuzo ya Academy Awards, ambayo filamu yake ilipigwa kwenye msitu wa mianzi wa Shunan? La pili, je, mji mdogo wa kale wa Lizhuang uko kwenye kando ya Mto Changjiang? Tunawakaribisha mshiriki kwa wingi, asanteni kwa kutusikiliza.