Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-11-20 16:42:29    
Mtu mashuhuri wa China ya kale Cao Cao na mashairi yake

cri

Kipindi cha Jian An kilichoanzia mwaka 196 hadi mwaka 220 mwishoni mwa Enzi ya Han Mashariki ni kipindi muhimu katika historia ya China. Katika kipindi hicho walijitokeza washairi wakubwa kama Cao Cao, Cao Pi na Cao Zhi, ambao walichangia ustawi wa fasihi ya China na kuipeleka katika kipindi kipya cha maendeleo. Katika kipindi hicho mashairi yalikuwa ya aina nyingi yakiwemo mashairi ya kueleza simanzi, hasira na matumaini ya maendeleo. Watu wa baadaye wameipa fasihi ya kipindi hicho jina la "fasihi ya Jian An". Mtu aliyejulikana zaidi katika kipindi hicho anaitwa Cao Cao.

Cao Cao alizaliwa mwaka 155 na kufariki mwaka 220 katika Enzi ya Han Mashariki. Kutokana na werevu alio nao, Cao Cao alipokuwa na umri wa miaka 20 aliingia ndani ya kasri la mfalme na kuwa ofisa mkubwa. Katika vita vingi dhidi ya wavamizi aliwashinda maadui akawa jemadari hodari, baadaye alikuwa mtawala halisi badala ya mfalme kutokana na mfalme wake alikuwa mnyonge, kwa hiyo baada ya yeye kufariki alipewa heshima ya kifalme na mtoto wake Cao Pi aliyekuwa mfalme wa Dola la Wei.

Cao Cao alikuwa ni mwanasiasa mkubwa, na mtaalamu wa mbinu za kivita, aliwashinda madiwani wengi waliojitenga na utawala wa mfalme na kuifanya sehemu ya kaskazini ya China iwe mikononi mwake. Cao Cao pia ni mshairi mkubwa, licha ya kupambana na maadui wa nje pia alistawisha fasihi, kwamba alijitahidi kukusanya wasomi, na huku akijiendeleza katika utunzi wa mashairi. Kutokana na juhudi hizo fasihi katika kipindi cha Jian An ilikuwa imestawi haraka ingawa jamii ilikuwa katika hali ya msukosuko kutokana na vurugu za vita zilizoendelea muda mrefu.

Cao Cao alikuwa ni mtu mwenye elimu nyingi katika fasihi na muziki. Uhodari wake wa fahisi unaonekana zaidi katika mashairi yake. Mashairi yake yaliyohifadhiwa hadi leo ni zaidi ya 20, mashairi hayo ni mepesi kuelewa na yanagusa hisia za watu kwa nguvu. Mashairi yake yanaweza kugawanyika katika aina tatu, moja ni ya kueleza msukosuko wa jamii mwishoni mwa Enzi ya Han Mashariki na maisha mabaya ya wananchi. Mashairi ya aina hiyo huwa yanaandikwa kwa maneno matano kwa kila beti na maneno yaliyotumika ni mepesi kueleweka, hali ya maisha iliyoelezwa katika mashairi hayo ni wazi kama inavyoonekana mbele ya macho ya watu. Aina nyingine ni mashairi yanayoeleza matilaba yake na moyo wa kujitakia maendeleo. Mashairi ya aina hiyo yaliandikwa kwa maneno manne kwa kila ubeti. Zaidi ya aina hizo Cao Cao pia aliandika mashairi yaliyoeleza hisia zake alizokuwa nazo alipokuwa katika utalii.

Mashairi katika kipindi cha Jian An kilichoanzia mwaka 196 mpaka mwaka 220 yanasifika katika historia ya mashairi ya China kwa sababu mashairi katika kipindi hicho yalijaa ukakamavu wa kiume, ukarimu na masikitiko, na hayo yanaonekana zaidi katika mashairi ya Cao Cao, mfano ni shairi lake la "Wimbo Mfupi".

Shairi hilo alilitunga katika usiku wa kabla ya kuipata China nzima baada ya kupata sehemu yote ya kaskazini na tayari kuvuka mto kuwaangamiza watawala wa sehemu ya kusini ya China. Katika usiku huo hali ya hewa ilikuwa nzuri, mbingu ilikuwa safi na mwezi ukining'inia angani. Ndani ya mashua mbele ya askari na majemadari waliojizatiti vizuri, alijawa na msukumo akaimba shairi hilo. Kwenye mwanzo wa shairi hilo lilisema, "Furaha ya kunywa pombe pamoja na muziki ni mara chache mtu anayoipata maishani mwake" ikimaanisha maisha ya binadamu ni mafupi, na muda unapita haraka kama mshale. Katikati ya shairi hilo alisema, "wasomi nawatamani usiku na mchana", ikionesha moyo wake wa kupenda na kutaka sana watu hodari kumsaidia. Na kwenye mwisho wa shairi hilo alisema, mtu anayewatendea vema wasomi ndiye mtu anayeweza kupata uungaji mkono wa watu wote na kutimiza nia yake ya kuiunganisha China nzima.

Cao Cao licha ya kuwa shujaa wa kupigana vita pia ni shujaa katika historia ya mashairi ya China.