Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-11-20 16:37:40    
Miaka 30 ya mageuzi ya sekta ya uchapishaji nchini China

cri

Kwenye maonesho ya vitabu yaliyomalizika hivi karibuni huko Frankfurt, Ujerumani, China imealikwa kuwa nchi mgeni muhimu itakayoshiriki kwenye maonesho yatakayofanyika mwaka kesho. Tokea China ilipokumbwa na uhaba wa vitabu mpaka kuwa nchi mgeni muhimu itakayoshiriki kwenye maonesho hayo makubwa ya vitabu duniani, hali hii imedhihirisha wazi kwamba China imepata maendeleo makubwa katika mageuzi ya sekta ya uchapishaji katika miaka 30 iliyopita.

Maonesho ya vitabu ya Frankfurt ni makubwa na ni biashara kubwa ya vitabu duniani. Kwenye maonesho hayo ya 60 yaliyofungwa hivi karibuni, naibu mkurugenzi wa Mamlaka ya China ya Uchapishaji wa Magazeti na Vitabu Bi. Li Dongdong alikabidhiwa na Uturuki ambayo ni nchi mgeni muhimu kwenye maonesho ya mwaka huu, kifurushi cha hati kilichoviringishwa ambacho ni alama ya nchi mgeni muhimu katika maonesho ya mwaka kesho. Bi. Li Dongdong alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema,

"Mwaka 2009 China ikiwa nchi mgeni muhimu itashiriki kwenye maonesho ya vitabu ya Frankfurt, hii ni mara ya kwanza kwa China kupata heshima hiyo. Katika maonesho hayo China itaonesha vitabu vyake vya aina zaidi ya 5,000. Vitabu hivyo licha ya kuonesha maendeleo ya shughuli za uchapishaji pia ni kielelezo cha kuonesha mafanikio makubwa yaliyopatikana katika mageuzi nchini China miaka 30 iliyopita.

Katika miaka 10 ya "Mapinduzi Makubwa ya Utamaduni" toka mwaka 1966 hadi mwaka 1976 nchini China, hali ya utamaduni ilizorota, ambapo mashirika mengi ya uchapishaji yalifungwa. Baada ya kipindi hicho kumalizwa, kiu ya wananchi ya kutaka kusoma vitabu ilikuwa kali, lakini mashirika ya uchapishaji yalishindwa kukidhi mahitaji yao. Naibu mwenyekiti wa Shirikisho la Wachapishaji la China Bw. Yang Deyan alipokumbusha hali ya wakati huo alisema,

"Baada ya China kuanza kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango mwishoni mwa mwaka 1978, wachina wengi walikuwa na hamu ya kujifunza lugha za kigeni ili kuwasiliana na nchi za nje, lakini wakati huo ulikuwa ni miaka ya uhaba wa vitabu. Nakumbuka kwamba watu kiasi cha elfu kumi hivi walisimama foleni kwa ajili ya kununua 'Kitabu cha Masomo ya Kiingereza' kilichohaririwa na Prof. Xu Guozhang, lakini waliopata walikuwa wachache kutokana na vitabu vichache vilivyouzwa kila siku. Wakati huo wanafunzi waliojifunza Kiingereza walikuwa hawana vitabu wala kamusi, sababu ni kuwa vitabu vilikuwa havijaandikwa, karatasi zilikuwa hazitoshi na uwezo wa uchapaji ulikuwa mdogo."

Wakati huo Bw. Yang Deyan alifanya kazi katika Shirika la Uchapishaji la Biashara. Shirika hilo lilianzishwa mwishoni mwa karne ya 19, ni shirika linaloshughulika zaidi na uchapishaji wa vitabu vya Magharibi. Ili kukidhi mahitaji ya wananchi wanaotaka kujifunza lugha za kigeni, shirika hilo lilichapa kazi usiku na mchana. Bw. Yang Deyan alisema,

"Mwaka 1978 shirika letu liliwasiliana na Shirika la Uchapishaji la Chuo Kikuu cha Oxford, baadaye tulichapisha kamusi ya Oxford. Hii ni kamusi ndogo ya Kiingereza-Kichina na Kichina-Kiingereza."

Bw. Yang Deyan alisema, Shirika la Uchapishaji la Biashara lilipita mchakato kutoka hali mbaya hadi hivi leo ambapo linachapicha vitabu vya aina nyingi kila mwaka. Aliongeza, baada ya maendeleo ya miaka 30, shughuli za uchapishaji nchini China zimestawi sana.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Uchapishaji wa Magazeti na Vitabu, mwaka 1978 aina za vitabu zilikuwa zaidi ya elfu kumi, mwaka 2007 aina za vitabu zilifikia laki mbili na elfu 40, majarida yaliyochapishwa mwaka 1977 yalikuwa ya aina 600, hadi mwaka jana aina zake zilifikia zaidi ya 9000, na magazeti yameongezeka kutoka aina 200 mwaka 1977 hadi kufikia aina 2000 mwaka jana na karatasi zilizotumika katika uchapaji zilikuwa shiti bilioni 40. Kadhalika, diski za CD na VCD mwaka 1978 zilikuwa milioni 30, na mwaka 2006 zilifikia milioni 460.

Baada ya miaka 30 ya maendeleo, China imeaga historia ya uhaba wa vitabu, hivi leo watu wanafurahia vitabu vingi kama bahari. Wageni wanaoishi nchini China pia wameshuhudia hali hiyio. Bi. Anna wa Russia amekuja nchini China katika miaka ya 90 ya karne iliyopita, ameishi nchini China kwa zaidi ya miaka kumi. Alisema,

"Kadiri China inavyoendelezwa, machapisho kutoka lugha za kigeni pia yanaongezeka, hususan miaka ya karibuni machapisho hayo yemekuwa mengi mno. Nakumbuka kwamba katika miaka ya 90 ya karne iliyopita, kwenye duka la vitabu sio kwamba naweza kupata kitabu maarufu cha Kirusi 'Vita na Amani' pia naweza kupata vitabu vingine vilivyoandikwa na waandishi wa vitabu wa zama hizi. Hivi sasa katika Jumba la Vitabu mjini Beijing kuna sehemu maalumu inayouza vitabu vya Kirusi. Katika kipindi cha Michezo ya Olimpiki ya Beijing kila siku niliweza kupata toleo la siku hiyo la majarida na magazeti ya Kirusi. Hapa nchini China tunaweza kuagiza magazeti yote yaliyochapishwa nchini Russia."

Katika muda wa miaka 30 iliyopita, sheria kuhusu hakimiliki ya kunakili imekamilika kimsingi, na mfumo wa kulinda hakimiliki hiyo umeanzishwa kisheria na kiutawala, kwa mfano, mwaka 2007 tu machapisho ya kurudufishwa yaliyogunduliwa na kuteketezwa na idara za kusimamia hakimiliki ya kunakili yalikuwa milioni 70, kati ya machapisho hayo, vitabu vilikuwa milioni 10.

Bw. Zheng Yuanjie ni mwandishi wa vitabu aliyeandika vitabu vingi, kitabu chake cha watoto kinauzwa haraka bila kupungua katika miaka zaidi ya 20 iliyopita, anaona kuwa hifadhi ya hakimiliki ya kunakili imehamasisha juhudi za waandishi wa vitabu. Alisema,

"Mwaka 1981 kitabu changu cha kwanza kilipotolewa, wizi wa hakimiliki ya kunakili ulikuwa haujatokea sana, lakini muda si mrefu baadaye wizi huo uliongezeka na kukithiri, hususan mwaka 1991 na mwaka 1992 ambapo wizi huo ulipamba moto. Nakumbuka kwamba wakati huo ingawa serikali ilifanya juhudi kubwa lakini ufanisi haukuwa kama ulivyotarajiwa, baadhi ya wandishi wa vitabu walikuwa hawataki kuandika kitu kutokana na wizi huo. Hivi sasa wamekuwa na juhudi kwa sababu hakimiliki yao ya kunakili inalindwa kisheria."

Katika miaka 30 iliyopita China imezidi kuzifungulia mlango nchi za nje katika sekta ya uchapishaji. Mwaka 1992 China ilijiunga na "Makubaliano ya Berne ya Hifadhi ya Hakimiliki ya Kunakili ya Maandishi na Sanaa" na "Makubaliano ya hakimiliki ya Kunakili Duniani". Mwaka 2003 China ikitimiza ahadi yake iliyotoa wakati ilipojiunga na shirika la biashara duniani WTO, ilifungua soko lake la uchapaji na usambazaji wa machapisho kwa nchi za nje, hatua za kushirikiana na nchi za nje katika sekta ya uchapishaji ziliharakishwa. Katika maonesho makubwa ya vitabu ya kimataifa, China imekuwa nchi isiyoweza kukosekana.

Kwenye maonesho ya 15 ya vitabu ya kimataifa yaliyomalizika hivi karibuni mjini Beijing, naibu mkurugenzi wa Mamlaka ya Uchapishaji wa Magazeti na Vitabu Bw. Yan Xiaohong alisema, China itaendelea kuleta mazingira mazuri kwa ajili ya ushirikiano wa uchapishaji kati ya China na nchi za nje. Alisema,

"China itazidi kuhamasisha mashirika ya uchapishaji ya China ili kupanua eneo la ushirikiano na itazidi kutilia nguvu mapambano dhidi ya wizi wa hakimiliki ya kunakili."

Idhaa ya kiswahili 2008-11-20