Mawaziri wa kilimo wa nchi 27 za Umoja wa Ulaya baada ya kufanya majadiliano makubwa kwa saa 18, walifikia makubaliano tarehe 20 huko Brussels kuhusu kufanya mageuzi juu ya sera za umoja huo za utoaji ruzuku ya kilimo, ambapo utoaji huo wa ruzuku ya kilimo utapunguzwa na kuongezwa mgao wa uzalishaji wa maziwa, hayo ni mafanikio muhimu tangu Umoja wa Ulaya unuie kufanya mageuzi kwa mara ya 5 kuhusu sera za kilimo mwaka 2003.
Sera za kilimo za Umoja wa Ulaya ni sera za kwanza zinazotekelezwa katika umoja huo, na ni hatua ya kwanza ya umoja huo ya kuelekea kwenye utandawazi wa shughuli za uzalishaji mali, ambazo zilianza kutekelezwa kwa zaidi ya miaka 40 iliyopita. Sera hizo zinahusu zaidi kutoa uungaji mkono kwa uwekaji bei ndani ya umoja huo na kuweka vizuizi vya biashara kwa nchi zisizo za umoja huo. Hivi sasa kila mwaka Umoja wa Ulaya unatumia Euro zaidi ya bilioni 42 kwa kutoa ruzuku na kuhamasisha usafirishaji bidhaa kwa nchi zisizo za umoja huo, kiasi hicho cha fedha ni karibu nusu ya bajeti ya umoja huo. Ingawa sera hizo zimetimiza lengo la kudumisha maendeleo ya uzalishaji wa kilimo na kulinda maslahi ya wakulima wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, lakini pia yalitokea matatizo mengi. Ugawaji wa maslahi usio wa usawa umesababisha mapambano ndani ya umoja huo; kuongezeka kwa mfululizo kwa matumizi ya fedha kutokana na ongezeko la nchi wanachama wapya kumekuwa mzigo mkubwa; vizuizi vingi vya biashara vilivyowekwa kwa nje vimedhoofisha nguvu za ushindani za kilimo cha Umoja wa Ulaya; sera za utoaji ruzuku ya kilimo zimesababisha hali isiyofaa ya biashara ya mazao ya kilimo duniani, ambayo imekwamisha maendeleo ya mazungumzo ya duru la Doha ya WTO. Baada ya kufanya mageuzi kwa mara 4, mwaka 2003 baraza la mawaziri wa kilimo la Umoja wa Ulaya lilitoa pendekezo kwa mara ya 5 la kufanya mageuzi kuhusu sera za kilimo za pamoja, lakini mageuzi hayo yanakabiliwa na changamoto nyingi, kutokana na kuhusika na ugawaji wa maslahi kati ya nchi wanachama na maslahi ya wakulima wapatao milioni 13.
Mageuzi ya safari hii ni kuhusu pande mbili. Upande wa kwanza ni dhidi ya mashamba makubwa, utoaji ruzuku ya kilimo kwa mashamba makubwa yenye mali zaidi ya Euro laki 3 kila moja, utapunguzwa kwa 10%, ili kutenga fedha nyingi zaidi kwa hifadhi ya mazingira ya asili. Upande wa pili, ni kuinua hatua kwa hatua viwango vya uzalishaji wa maziwa vya nchi wanachama, na viwango vya uzalishaji vilivyowekwa vitafutwa kabisa mwishoni mwa mwezi Machi mwaka 2015.
Kutokana na mapatano hayo, mkutano huo umeamua kutekeleza hatua hizo za mageuzi toka mwaka 2009 hadi mwaka 2013. Mjumbe wa kamati ya maendeleo ya kilimo na vijiji ya Umoja wa Ulaya, Bi. Mariann Fischer Boel amekiri kuwa mapatano hayo ni matokeo ya usuluhisho, vilevile alisema, "kila nchi mwanachama imetoa mchango, na kila nchi mwanachama imepata manufaa, kweli haikuwa rahisi kufanikisha mapatano hayo! Kimsingi, makubaliano hayo yananufaisha mustakabali wa Umoja wa Ulaya."
Kutokana na kuwepo kwa tofauti ya matakwa ya nchi wanachama za umoja huo, hivyo maoni yao kuhusu mafanikio ya makubaliano hayo pia ni tofauti sana. Mchambuzi anasema, kutokana na mageuzi ya sera za kilimo, Umoja wa Ulaya unaweza kupunguza migongano ya ndani, kuimarisha nguvu za ushindani wa mazao ya kilimo na kupunguza shinikizo inayotoka jumuiya ya kimataifa ya kukosoa sera zake za biashara. Lakini sera hizo zitaweza kutekelezwa ipasavyo au la bado haijulikani sasa, kwani sera hizo zinahusika na maslahi ya wakulima wa nchi wanachama 27. Kufanya mageuzi katika hali ngumu ya hivi sasa duniani huenda kutakuta taabu kubwa zaidi .
|