Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-11-21 19:17:14    
Hadithi ya mfanyabiashara wa Taiwan aliyeanzisha kampuni yake katika China bara

cri

Mkoa wa Fujian ulioko kusini mashariki mwa China unapakana na kisiwa cha Taiwan. Mazingira ya kijiografia, hali ya hewa na desturi za sehemu hiyo mbili zinafanana. Meneja wa kampuni ya viatu ya Yuesheng ya Fuzhou Bw. Wang Jiankun ni mfanyabiashara wa Taiwan mwenye asili ya mkoa wa Fujian. Kuanzisha shughuli zake katika China bara ni matumaini yake tangu zamani. Hivi sasa ametimiza ndoto yake, kwa sababu ameanzisha kampuni yake mjini Fuzhou, na bidhaa za kampuni yake zinauzwa duniani.

China ina utamaduni unaong'ara, historia ya miaka elfu kadhaa imeiacha mabaki mengi ya kihistoria na mali za urithi wa utamaduni katika China bara. Kutokana na sababu hiyo, watu wengi wana matumaini ya kuja China bara, akiwemo Bw. Wang Jiankun. Bw. Wang alisema,

"Nilitamani sana kuja China bara. Katika miaka ya 80 ya karne iliyopita, nilifikiri kuwa siku moja nitakuja China bara, na nilitimiza ndoto yangu katika mwaka 1990."

Katika mwaka 1990 mawasiliano ya kiuchumi na kiutamaduni kati ya China bara na Taiwan yalikuwa yameongezeka siku hadi siku, China bara ilifungua mlango na kutoa sera mbalimbali za kuwanufaisha wafanyabiashara wa Taiwan. Kutokana na hali hii, Bw. Wang Jiankun na mfanyabiashara mwingine wa Taiwan walifika mji wa Shenzhen ambao ulitangulia kutekeleza sera ya mageuzi na ufunguaji mlango. Wakati huo Bw. Wang Jiankun alikuwa bado hajafikia umri wa miaka 40.

Baada ya kufahamu sera ya China bara ya kuwanufaisha wafanyabiashara wa Taiwan, mwaka 1993 alikwenda mji wa Fuzhou mkoani Fujian. Wakati huo makampuni ya kiserikali ya China yalianza kufanya mageuzi, na makampuni binafsi yalipata maendeleo makubwa. Bw. Wang Jiankun akitumia fursa hiyo, alianzisha kampuni ya viatu ya Yuesheng mjini Fuzhou. Bw. Wang alisema,

"Katika miaka mitatu baada ya kuja China bara, nilipata maarifa mengi kuhusu njia za kuanzisha kampuni katika China bara, kupata orodha za uagizaji huko Taiwan, kutengeneza bidhaa hapa China bara, na kupeleka bidhaa kupitia Hongkong."

Bw. Wang Jiankun anawaheshimu zaidi watu wawili, mmoja ni Marehemu Mao Zedong, na mwingine ni mutu mashughuri wa mkoa wa Fujian katika zama za kale Wang Shenzhi. Bw. Wang Jiankun anaona kuwa mawazo ya watu hao wawili yamesaidia sana shughuli zake.

Katika kabati iliyoko ofisini mwa Bw. Wang Jiankun, kuna sanamu mbalimbali za Marehemu Mao Zedong. Bw. Wang Jiankun alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa amezoea kutumia mawazo ya Marehemu Mao wakati anaposimamia kampuni yake. Anaona kuwa katika mambo ya usimamizi Marehemu Mao alikuwa na uwezo wa kuchambua mambo makuu na yasiyo muhimu, akishika masuala makuu, kuyachambua na kuyatatua. Aidha, Marehemu Mao alishikilia kanuni mbalimbali na kuzingatia unyumbufu wa mikakati. Maarifa hayo yanamsaidia sana Bw. Wang Jiankun wakati aliposimamia kampuni yake.

Mwaka 2003, ugonjwa wa SARS uliambukiza katika China bara. Shughuli za kampuni ya Bw. Wang Jiankun ziliathiriwa vibaya. Baada ya kukata tamaa kwa muda mfupi, alitiwa moyo tena. Alisema wakati huo alimkumbuka Marehemu Mao ambaye aliyashinda matatizo kwa akili na ushujaa wake na kupata ushindi mwishowe. Baada ya kufikiri hali ya wakati huo, Bw. Wang Jiankun aliamua kuwapa wafanyakazi mafunzo wakati kampuni yake haikuweza kufanya kazi. Bw. Wang alisema,

"Nilitumia fursa hiyo kuwapa wafanyakazi mafunzo. Katika mwaka wa pili, kampuni yangu ilikuwa na wafanyakazi hodari."

Kuna usemi wa Kichina usemao, "kunoa panga kabla ya kukata kuni hakutapoteza wakati wowote." Kampuni ya viatu ya Yuesheng ilitoa mafunzo kwa wafanyakazi wake, na kuweka msingi imara wa kuinua uwezo wa wafanyakazi na kuhimiza maendeleo ya kampuni hiyo.

Mtu mwingine anayemathiri Bw. Wang Jiankun ni mtu mashughuri wa Fujian katika zama za kale Wang Shenzhi. Mwaka 897 katika enzi ya Tang, Wang Shenzhi alikuwa ofisa wa serikali mjini Fuzhou. Wakati huo Wang Shenzhi alitekeleza sera ya kulinda ardhi, kuhakikisha usalama wa wakazi, kuchagua watu hodari kuwa watumishi wa serikali, kutilia maanani uzalishaji, kuanzisha shule, na kujenga mradi wa kuhifadhi maji mashambani. Kutokana na hatua hizo, wakazi wa huko waliishi katika hali ya usalama, na walimheshimu sana Wang Shenzhi.

Bw. Wang Jiankun ameathiriwa na Wang Shenzhi. Wafanyakazi wa kampuni yake wanaona kuwa yeye ni mpole na mwenye akili. Ofisa wa idara ya uhasibu ya kampuni yake Bi. Yin alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema,

"Mwaka juzi sisi tulifanya kosa ambalo lilikuwa nusura kuleta hasara zaidi ya yuan milioni 1 kwa kampuni yetu, lakini meneja wetu mkuu hakutukosoa. Tunafurahi sana, yeye ni mtu mwema."

Baada ya kushindana kwenye soko la Fuzhou kwa miaka kadhaa, Bw. Wang Jiankun alipata maarifa mengi kuhusu uzalishaji, usimamizi na uuzaji, na kampuni yake ilipata maendeleo makubwa. Aliposhughulikia biashara ya nje, alifanya ukaguzi kuhusu masoko, na kutengeneza bidhaa zinazokidhi mahitaji ya masoko. Miaka mitatu baada ya kampuni yake kuanzishwa, mapato ya kampuni yake yaliongezeka kwa mara tatu, idadi ya wafanyakazi iliongezeka kuwa zaidi ya elfu 2 kutoka mia 3, na Bw. Wang Jiankun alichaguliwa kuwa naibu mkurugenzi wa shirika la viwanda na biashara la eneo la Jin'an la Fuzhou na naibu mkurugenzi wa shirika la uwekezaji la wafanyabiashara wa Taiwan mjini Fuzhou.

Bw. Wang Jiankun hajaridhika na mafanikio ya hivi sasa, lengo lake ni kuuza bidhaa za kampuni yake zinazoweza kuwaridhisha wateja duniani. Bw. Wang alisema,

"Kampuni yangu ilipata maendeleo ya haraka. Jina la kampuni yangu ni Yuesheng, ambalo linamaanisha kuruka, hivyo ilipata maendeleo makubwa kama inaruka juu. Kampuni yangu inashughulikia biashara ya nje, bidhaa zetu zinauzwa nchini Marekani na Canada, ambayo ni masoko makubwa."

Mwaka jana viatu vya michezo vya chapa ya Dashayu vilivyotengenezwa na kampuni ya Yuesheng kwa kushirikiana na kampuni ya mchezaji maarufu wa gimnastiki wa China Bw. Li Ning viliuzwa vizuri kwenye soko la Marekani. Hivi sasa maduka zaidi ya elfu 20 nchini Marekani yanauza bidhaa zao, na kila mwaka viatu zaidi ya milioni 10 vinauzwa nchini humo.