Makundi ya waasi yasaini makubaliano ya mazungumzo ya amani Sudan.
Makundi mawili hasimu ya waasi na serikali ya Sudan wametia saini kwenye makubaliano ya mazungumzo ya amani Darfur. Makubaliano hayo yamefikiwa siku ya Alhamisi wiki hii katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin.
Makubaliano hayo yaliidhinishwa na makundi mawili ya waasi JEM na SLA-MM pamoja na Amin Hassan al Omari, mwenyekiti wa Mazungumzo kwa upande wa serikali ya Sudan.
Mazungumzo hayo yalifanyika chini ya mwamvuli wa Umoja wa Afrika, akiwepo rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, ambaye anaongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa Umoja wa Afrika katika kushughulikia migogoro ya Sudan.
Mkataba huu ni hatua ya kwanza kuelekea mchakato mpya wa mazungumzo kati ya makundi tofauti katika mgogoro Darfur.
Kiongozi wa kundi kuu la waasi la JEM Gibril Ibrahim amesema mkataba huo unaandaa hatua zijazo.
Kwa mujibu wa msemaji wa JEM, mkataba huu wa "nia nzuri" utafuatiwa na mwingine ambao utasitisha mapigano, na wa tatu ambao utatoa ratiba ya mazungumzo ya kukomesha vita vya tangu mwaka 2003 katika Sudan ya magharibi.
Umoja wa Afrika, ambao ni mpatanishi katika suala hili kwa miaka mitatu, ulifaulu kuzikutanisha pande mbalimbali katika mazungumzo bila masharti yoyote.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |